Marekani: Lebanon si sehemu ya makubaliano ya kusitisha vita
9 Aprili 2026
Rais wa Marekani Donald Trump amesema Lebanon si sehemu ya makubaliano ya kusitisha mapigano kwa wiki mbili yaliyoafikiwa, akiliita suala la Lebanon kuwa mzozo tofauti, huku Israel ikifanya wimbi kubwa la mashambulizi dhidi ya Lebanon baada ya makubaliano hayo kutangazwa.
Iran kwa upande wake imesema itakomesha usitishaji mapigano kwa upande mmoja ikiwa mashambulizi ya Israel yataendelea dhidi ya Lebanon.
Wizara ya afya ya Lebanon imetangaza idadi ya vifo kutokana na mashambulizi makubwa ya Israeli jana Jumatano kuwa watu 182, idadi inayoelezwa kuwa kubwa zaidi ya vifo vya siku moja tangu mzozo wa hivi karibuni na Israeli ulipoanza Machi 2.
Wizara hiyo iliongeza kusema watu 890 wamejeruhiwa. Takwimu kutoka kwa huduma ya ulinzi wa raia ya Lebanon mapema ilitangaza idadi ya vifo kuwa 254.
Waziri mkuu wa Lebanon Nawaf Salam alitangaza Jumatano jioni kwamba leo Alhamisi itakuwa siku ya maombolezo kwa wote waliouawa.
Wakati huo huo, kamati ya kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) ilisema imekasirishwa na vifo na uharibifu huo mbaya.
Mkuu wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, Volker Türk, amelaani mashambulizi makubwa ya Israel dhidi ya Lebanon Jumatano. Türk alisema kabla ya Jumatano zaidi ya watu 1,500 walikuwa wameuawa katika mashambulizi ya Israeli tangu Machi 24, huku zaidi ya watu milioni moja wakilazimika kuyahama makwao. Alitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kukomesha ndoto hii mbaya.
Spika wa bunge la Iran asema makubaliano yamekiukwa
Spika wa bunge la Iran, , alisema kusitisha mapigano au mazungumzo ya pande mbili hayana mantiki huku akiorodhesha matukio matatu ya ukiukwaji wa kusitisha mapigano aliosema ulifanywa Jumatano.
Katika chapisho kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X, Qalibaf alisema mashambulizi ya Israel yanayoendelea dhidi ya Lebanon yalikiuka kifungu cha kwanza cha makubaliano ya kusitisha mapigano, akitoa mfano wa uthibitisho wa mpatanishi Pakistan. Israel na Marekani zimeshikilia kwamba Lebanon haijajumuishwa katika kusitisha mapigano.
Spika wa Iran pia aliorodhesha mwisho wa mashambulizi dhidi ya Iran na haki ya Iran ya kujitajirisha kama vifungu vingine viwili, akisema ndege isiyo na rubani iliharibiwa katika anga ya mji wa Lar nchini Iran katika jimbo la Fars licha ya kusitisha mapigano.
Shirika la habari la Reuters lilinukuu vyanzo vya Pakistani ambavyo havikutajwa majina vikisema Qalibaf pamoja na waziri wa mambo ya nje Abbas Araghchi ambao wataelekea Islamabad kwa mazungumzo na Marekani.
Iran hvi leo imetangaza njia mbadala kwa meli zinazosafiri kupitia mlango bahari wa Hormuz, ikitaja hatari ya mabomu ya baharini katika eneo kuu la njia muhimu ya maji.
Netanyahu asema Israel iko tayari kurudi vitani
Wakati haya yakiarifiwa, waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema Israel iko tayari kurudi vitani baada ya kutangazwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano na Iran. Netanyahu alisema katika taarifa iliyorushwa kwenye televisheni na hapa tunanukuu: "Niweke wazi: Bado tuna malengo ya kukamilisha, na tutayafikia - ama kupitia makubaliano au kupitia mapigano mapya," mwisho wa kunukuu.
Netanyahu pia alisisitiza kwamba makubaliano hayo yalikubaliwa kwa uratibu kamili na Israel, akisema hawakushangazwa wakati wa mwisho na tangazo hilo.
Trump aikosoa jumuiya ya NATO
Ikulu ya White House hapo jana ilisema rais Trump anaamini jumuiya ya kijeshi ya NATO ilijaribiwa na walishindwa wakati wa vita vya Iran, kabla ya mkutano kati yake na katibu mkuu wa jumuiya hiyo, Mark Rutte.
Trump aliikosoa NATO na alionekana kufufua vitisho vyake kuhusu kisiwa cha Greenland baada ya mkutano wa faragha na Rutte, ambapo alitarajiwa kujadili uwezekano wa kuondoka katika kambi hiyo muhimu ya usalama baada ya kushindwa kujiunga na vita vya Iran.
Trump alikuwa akiangalia njia mbadala ya kuwaadhibu baadhi ya wanachama wa NATO ambao aliamini hawakuwa na msaada wakati wa mzozo kwa kuwahamisha wanajeshi wa Marekani kutoka nchi zao, Wall Street Journal iliripoti.