1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yasema shutuma za Korea Kaskazini ni "upuuzi "

Isaac Gamba
26 Septemba 2017

Marekani imezitaja kuwa upuuzi mtupu shutuma zilizotolewa na Korea Kaskazini kwamba Rais Donald Trump ametoa tangazo la kuashiria vita dhidi ya utawala wa nchi hiyo .

Donald Trump
Picha: picture-alliance/AP Photo/B. Anderson

 Shutuma hizo zimetolewa na  waziri wa mambo ya nje wa Korea Kaskazini Ri- Yong-ho alipozungumza na waandishi wa habari mjini New York kuhusiana na   ujumbe wa mwishoni mwa wiki wa Rais Donald Trump kupitia ukurasa wa twitter kuwa uongozi wa  Korea Kaskazini "hautadumu kwa muda mrefu" iwapo utaendelea na vitendo vyake vya uchukozi.

Ri, aliyehudhuria mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa wa mwaka huu amesema Jumuiya ya kimataifa ina matumaini kuwa vita vya maneno havitageuka kuwa "vita vya kweli".  Hata hivyo Marekani  kupitia kwa msemaji wa ikulu ya Rais ya White House Sarah Huckabee Sanders imepinga tafsiri hiyo ya Korea Kaskazini kuhusiana na kauli aliyotoa Trump  na kusema hawajatangaza vita dhidi ya Korea Kaskazini na kusisitiza kuwa tafsiri hiyo ya Korea Kaskazini ni upuuzi mtupu.

Mjadala kuhusiana na mpango wa silaha za nyukilia na makombora ya Korea Kaskazini  ulitawala mkutano wa mwaka huu wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa huku majibizano ya maneno makali kati ya Marekani na Korea Kaskazini yakisababisha hofu kuwa yasije yakachochea vita.

Makali ya hofu hiyo yalizidi kuongezeka hasa baada ya ndege za kivita za Marekani kuruka kuelekea mwambao wa Korea Kaskazini Jumamosi iliyopita na kwenda kaskazini zaidi katika ukanda usio na mazingira ya kivita ambako ndege za Marekani hazijawahi kuruka katika karne hii.

 

Korea Kaskazini yasema ina haki ya kujibu kitakachotokea dhidi yake

Waziri wa mambo ya nje wa Korea Kaskazini Ri Yong HoPicha: picture-alliance/AP Photo/J. Jacobson

Waziri wa mambo ya nje wa Korea Kaskazini  ,Ri Yong Ho  alisema kwa vile Marekani imetangaza vita dhidi yao watakuwa na kila haki ya kujibu kitakachotokea ikiwa ni pamoja na kudungua ndege za kivita za kimakakati za Marekani  hata kama ndege hizo haziko katika eneo la anga  la mpaka wa nchi hiyo na hivyo swali la kuwa nani au uongozi gani hautakaa kwa muda mrefu litakuwa limejibiwa.

Idara ya usalama  ya Korea Kusini (NIS) imesema wakati Korea Kasakazini ikiwa haoneshi kuwa imetumia hatua ya  ndege za kivita za Marekani kurushwa katika ukanda huo mwishoni mwa wiki lakini bado ilikuwa imechukua hatua za kuimarisha ulinzi katika ukanda wake wa pwani.

Wakati vita hivyo vya maneno vikizidi kushika kasi,  Korea Kusini imetoa mwito wa kupunguza mvutano uliopo huku waziri wa mambo ya nje wa Korea Kusini Kang Kyung- wha akisema vitendo vya uchokozi zaidi kutoka Korea Kaskazini vinaeza kutarajiwa lakini havipaswi kuruhusiwa kufikia hatua ya kushindwa kudhibitiwa.

"Ni muhimu kuwa sisi, Korea na Marekani tunadhibiti hali hii kwa pamoja ili kuzuia  kuongezeka kwa mvutano au aina yoyote ya mapambano ya kivita ambayo yanaweza kufikia haraka katika hatua ya kushindwa kudhibitiwa" alisema waziri wa mambo ya nje wa Korea Kusini.

China leo imeonya kuwa mzozo katika rasi ya Korea hautakuwa na mshindi ikiongeza kuwa inatumai Marekani na Korea Kaskazini zitagundua kuwa vita vyao vya maneno vitaonegza tu mzozo uliopo na kupuguza fursa za kupatikana suluhisho la kidiplomasia.

Mwandishi: Isaac Gamba/ AFPE

Mhariri : Caro Robi