1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yasema TPLF kuilenga Addis Ababa ni kitisho kikubwa

Daniel Gakuba
4 Novemba 2021

Kufuatia tangazo la Jumatano la kundi la ukombozi wa Tigray, TPLF kwamba limeuthibiti mji wa Kemissie ulio umbali wa kilomita 325 kutoka Addis Ababa, Marekani imesema hali hiyo itazidisha mzozo wa kibinaadamu Ethiopia.

Äthiopien Mekele | Pro-TPLF Rebellen
Wapiganaji wa kundi la TPLF wakitembea mjini Mekele baada ya wanajeshi wa serikali kuukimbiaPicha: YASUYOSHI CHIBA/AFP

Msemaji wa TPLF, Getachew Reda amesema hapo jana kuwa vikosi vya kundi hilo lililogeuka la uasi dhidi ya serikali ya shirikisho ya mjini Addis Ababa, vilikuwa vimefika katika mji wa Kemissie ulioko katika jimbo la Amhara, kilomita zipatazo 325 kaskazini mwa mji mkuu wa Ethiopia.

Getachew aliongeza kuwa wapiganaji wao walikuwa wakishirikiana na kundi jingine la uasi la Kioromo, OLA ambalo wiki hii lilitabiri kuwa mji mkuu Ethiopia unaweza kuangukia mikononi mwao katika muda wa miezi michache, au hata wiki tu.

Soma zaidi: Waziri mkuu Abiy aapa kuwazika maadui katika "damu yetu"

Afisa wa ngazi ya juu wa Shirika la Marekani la Msaada wa kimataifa, USAID amesema mjini Washington kuwa kusonga mbele kwa makundi ya waasi kuelekea Addis Abiba kunaweza kusababisha adha ya watu zaidi kuzikimbia nyumba zao, na kuongeza maumivu kwa watu wa Ethiopia.

Marekani yafuatilia kwa wasi wasi mkubwa

Naye msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Ned Price ameongeza kuwa Washington inaufuatilia mzozo wa Ethiopia kwa wasiwasi mkubwa.

Hali ya kibinadamu kaskazini mwa Ethiopia inazorota zaidi kila sikuPicha: EDUARDO SOTERAS/AFP/Getty Images

''Nataka kutamka wazi kuwa tunatiwa hofu na kukithiri kwa ghasia katika mzozo wa Ethiopia, na kupanuka kwa maeneo ya vita kaskazini mwa nchi hiyo na katika mikoa mingine. Tunahofia kukua kwa kitisho dhidi ya umoja na muungano wa Ethiopia kama taifa.'' Amesema Price.

Soma zaidi: Wakaazi wa Addis Ababa watakiwa kusajili silaha zao

Marekani imezitolea wito pande zote za mzozo huo kusitisha uhasama, na mjumbe wake maalumu kwa ajili ya Pembe ya Afrika Jeffrey Feltman anatarajiwa kuwasili mjini Addis Ababa leo Alhamis, katika ziara ya siku mbili yenye lengo la kupigia debe amani kwa njia ya mazungumzo.

Ubalozi wa Marekani mjini Addis Ababa umeruhusu wafanyakazi wake wanaotaka kuondoka Ethiopia kwa hiari yao kufanya hivyo, ingawa umesema kwa wakati huu hakuna anayelazimika kuondoka nchini humo.

Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed (kushoto) pamoja na Rais Yoweri Museveni alipoitembelea Uganda Agosti 2021.Picha: Lubega Emmanuel/DW

Marekani ni miongoni mwa mataifa ambayo yameikosoa sana mienendo ya serikali ya Ethiopia katika mzozo huu wa Tigray ambao umedumu kwa mwaka mmoja sasa.

Museveni aitisha mkutano wa viongozi wa Mashariki mwa Afrika

Wakati huo huo, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amewaalika viongozi wa kanda ya Afrika Mashariki kukutana tarehe 16 mwezi huu wa Novemba, kujadili hali ya mambo nchini Ethiopia.

Naibu waziri wa mambo ya nje wa Uganda Okello Oryem amesema Rais Museveni anawasiliana na waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, na amebainisha kusikitishwa kwake na hatua ya TPLF kukataa mazungumzo juu ya kusimamisha mapigano.

 

afpe, rtre

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW