Marekani yashauriwa kutoiachia pasifiki kwa China
20 Septemba 2022Ripoti ya wataalamu wa ushauri kutoka taasisi ya amani ya Marekani, ambayo waandishi wake wanahusisha maafisa wa juu wa zamani wa kijeshi, imesema China ilikuwa imepiga hatua katika kanda ya pasifiki kuhusu malengo ya kimkakati ya kieneo ambayo haijawahi kufanikisha kokote kwingine.
Ripoti hiyo imesema hali hii inasababisha wasiwasi ingawa siyo ya kuogofya, na kuongeza kuwa Marekani inapaswa kuimarisha msaada kwa mataifa ya visiwa katika eneo la kaskazini mwa Pasifiki ambako ina uhusiano imara zaidi wa kihistoria.
Soma pia: Marekani yaimarisha ulinzi wa makombora
Ripoti hiyo inakuja kabla ya mkutano kati ya rais wa Marekani Joe Biden na viongozi kadhaa wa mataifa ya visiwa vya pasifiki wiki ijayo, wakati ambapo Washington inawania ushawishi na Beijing katika eneo hilo.
Visiwa vya Marshall, shirikisho la mataifa ya Micronesia, pamoja na Palau, ni mataifa huru yanayojulikana kama Mataifa yalioungana kwa hiari, FAS, baada ya kusaini mapatano mwishoni mwa miaka ya 1980 ambayo yanaipa Marekani jukumu la ulinzi na haki ya kuweka vituo vya kijeshi.
Mapatano hayo, ambayo yanaisha muda wake mwaka 2023 na 2024, yanajadiliwa upya, na ripoti hiyo imeonya kwamba mataifa hayo huenda yakaigeukia China kwa ajili ya ufadhili endapo majadiliano yatashindwa.
Ripoti hiyo imesema eneo kubwa la bahari la mataifa ya FAS linalovuka sehemu kubwa ya pasifiki ya kaskazini, ni kizuwizi muhimu cha kimkakati kati ya miundombinu ya kiulinzi ya Marekani huko Guam na Hawaiipamoja na maeneo ya pwani ya Asia Mashariki.
Hatari kwa uwezo wa kijeshi wa Marekani
Waandishi wa ripoti hiyo ambao wanahusisha kamanda wa zamani wa kamandi ya Marekani ya Indo-Pasifiki Philip Davidson, pamoja na David Stilwell, naibu waziri wa zamani wa mambo ya nje, wameonya kuwa endapo China itafanikiwa kuliingiza mojawapo ya mataifa hayo katika ushawishi wake, hali hiyo itahatarisha uwezo wa kijeshi wa Marekani katika eneo hilo muhimu la kimkakati, na kufungua mlango wa mabadiliko makubwa katika miundombinu ya kikanda, kutakakokuwa na madhara yanayokwenda mbali ya kanda ya pasifiki.
Soma pia:Umoja wa Ulaya na nchi za ACP karibu kufikia makubaliano
Ripoti hiyo imesema katika kanda ya pasifiki, China inataka kuimarisha ufikiaji wake wa bandari na kanda maalumu za kiuchumi, kuvuruga juhudi za Marekani kuonesha nguvu ya kijeshi, kuongeza uwezo na ukusanyaji wa taarifa za kiintelijensia, kupunguza washirika wa kidiplomasia wa Taiwan, na kukuza ruwaza ya China ya maendeleo ya kisiasa na kiuchumi.
Washington inahitaji kutoa mbadala kwa msaada wa kiuchumi wa China ili kukabiliana na juhudi za Beijing kutumia hisia za kikanda za kutelekezwa. Rasilimali zaidi zinahitajika kufuatiali shughuli zinazoongezeka za China katika mataifa ya FAS, ambako meli za utafiti za China zenye vifa vya kijeshi zimeonekana bila ruhusa, imesema ripoti hiyo.
Mataifa ya shirikisho la Micronesia hivi karibuni yalikubali kujenga vituo vipya vya kijeshi vya Marekani, na Palau iliiomba Marekani kujenga viwanja vya ndege, bandari na kambi, ambavyo Washington inapaswa kuzingatia kwa uzito kiasi cha kutakiwa kuainisha maombo hayo na mahitaji yake ya kiulinzi.