1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yashutumu majasusi wa Urusi kudukua uchaguzi 2016

Sekione Kitojo
14 Julai 2018

Jopo la mahakama kuu jana Ijumaa(13.07.2018) limewashitaki maafisa 12 wa kijasusi wa Urusi kwa kudukua mtandao wa kompyuta wa chama cha Democratic mwaka 2016, katika shutumu zilizotolewa maelezo ya kina kutoka Marekani. 

US Sonderermittler Robert Mueller
Picha: Reuters/Y. Gripas

Hizi ni shutuma za kwanza  za  kina kuwahi  kufanyika katika  madai  ya  muda  mrefu  kwamba  Urusi iliingilia uchaguzi wa rais kumsaidia  mgombea wa chama cha  Republican  Donald Trump.

Rais Trump (kushoto) akiwa na waziri mkuu wa Uingereza Theresa May(kulia) wakati wa ziara nchini UingerezaPicha: Reuters/L. Marin

Mashitaka  hayo, ambayo ni  madai ya kula  njama katika  maeneo kadhaa yanayohusu udukuzi wa  hali  ya  juu  na  utoaji  wa  nyaraka , unazusha  hali  ya  wasi  wasi kwa  ajili  ya  mkutano  wa  kilele wiki  ijayo  baina ya  marais Trump  na  Vladimir Putin.

Maafisa  wa idara  ya ujasusi  katika  jeshi  la  Urusi, inayojulikana kama  GRU, kwa  chini  chini  walikuwa  wakichunguza kompyuta za kampeni  ya  mgombea  wa  chama  cha  Democratic  Hillary Clinton pamoja  na  kamati ya  kampeni  ya  chama  cha  Democratic, na kuiba idadi  kubwa ya  data, mashitaka  hayo  yamesema.

"Pamoja  na  kutoa  nyaraka  moja  kwa  moja  kwa umma, washitakiwa  walihamisha  nyaraka  zilizoibiwa  kwenda  katika shirika  lingine, ambalo  halikutajwa  katika  mashitaka  hayo, na kujadili muda  wa  kutoa nyaraka  hizo  katika  juhudi  za  kuongeza athari  katika  uchaguzi  huo," Naibu mwanasheria  mkuu  wa  serikali ya  Marekani  Rod Rosenstein aliwaambia  waandishi  habari.

Kushitakiwa  kwa  watu  hao  jana  Ijumaa (13.07.2018) kumekamilishwa  na  mshauri  maalum Robert Mueller kama  sehemu ya  uchunguzi  wake  kuhusiana  na  uhusika  wa  Urusi katika uchaguzi huo. Alikuwa kwanza  Mueller  ambaye moja  kwa  moja aliishitaki serikali  ya  Urusi kwa  kuingilia  uchaguzi, ambao  bila kutarajiwa Trump  alishinda. Serikali  ya  Urusi  inakana kuingilia  kati huko.

Rais Vladimir Putin wa UrusiPicha: Reuters/S. Bobylev

Trump afahamishwa

Rosenstein alisema  alimfahamisha  rais  Trump mapema  wiki  hii juu ya mashitakam  hayo. Hayana  madai  kwamba  raia  wa  Marekani walifanya  uhalifu, alisema.

Masaa machache  kabla  ya  mashitaka  hayo  kutangazwa, Trump aliuita uchunguzi  huo  wa  Mueller "utafutaji mchawi ulioghushiwa" ambao  unaathiri uhusiano  kati  ya  Marekani  na  Urusi.

Tangazo  hilo la  mashitaka limekuja  katika  wakati mbaya kwa Trump, ambaye  alikutana  na  malkia Elizabeth katika  kasri  la Windsor jana  Ijumaa  na  kunywa  nae  chai wakati  wa  ziara  yake nchini  Uingereza.

Trump  alisema , bila  shaka  atamuuliza  Putin juu ya  kuingilia wakati  watakapokutana  katika  mkutano  uliopangwa  kufanyika mjini  Helsinki siku  ya  Jumatatu.

Naibu mwanasheria mkuu wa serikali ya Marekani Rod RosensteinPicha: Reuters/A.-P. Bernstein

Wizara  ya  mambo  ya  kigeni  ya  Urusi  ilisema  jana  Ijumaa kwamba  mashitaka  hayo  yana  lenga katika  kuharibu hali  ya hewa  kabla  ya  mkutano  huo wa  kilele. Imesema  hakuna  ushahidi kwamba  watu  hao  12 walioshitakiwa  wanahusika  na  ujasusi katika  jeshi  ama  udukuzi.

Trump atakiwa kufuta mkutano

Wabunge  kadhaa  maarufu  wa  chama  cha  Democratic walimtaka Trump kufuta mkutano  wake  na  Putin.

"Kutokana  na mashitaka  haya  yaliyotolewa  na  idara ya  sheria kwamba  Warusi  hawa  walikula  njama kushambulia demokrasia yetu  na  walikuwa  wanawasiliana na Wamarekani kuingilia  kati uchaguzi  wetu, rais  Trump anapaswa bila  kusita  kufuta mkutano wake  na  Vladimir  Putin," alisema  seneta Jack Reed, seneta  wa ngazi  ya  juu  wa  chama  cha  Democratic katika  kamati ya huduma  za  jeshi  katika  baraza  la  seneti.

Kiongozi wa uchunguzi dhidi ya Urusi Robert MuellerPicha: picture-alliance/abaca/O. Douliery

Mueller  anachunguza  iwapo kampeni  ya  Trump ilishirikiana  na Urusi  na  iwapo rais alitafuta  kwa  njia ambayo  ni  kinyume  na sheria  kuzuwia  uchunguzi dhidi  ya  Urusi.

Mashirika  ya  ujasusi ya  Marekani  yalifikia hitimisho Januari mwaka  2017 kwamba  Urusi, ilifanya  juhudi  zilizoamrishwa  na  rais Putin, kutumia  propaganda  na  udukuzi  kuingilia  kati  uchaguzi kumuathiri  Clinton  na  hatimaye  kumsaidia  Trump  kushinda.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / rtre

Mhariri: Caro  Robi

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW