1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yasitisha ufadhili wake kwa Wapalestina

Caro Robi
1 Septemba 2018

Marekani imesema imesitisha ufadhili kwa shirika la Umoja wa Mataifa linalotoa misaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA, hatua inayotishia kuuzidisha mzozo kati ya Palestina na utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump.

Flüchlingslager Yarmouk bei Damaskus
Picha: picture-alliance/dpa

Msemaji wa Rais wa Palestina Mahmoud Abbas amelaani uamuzi huo alioutaja kama hatua ya kuwadunisha Wapalestina na inayoendana kinyume na maazimio ya Umoja wa Mataifa.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani Heather Nauert amesema operesheni na muundo wa shirika hilo la UNRWA una mapungufu makubwa na baada ya tathmini ya kina, Marekani imeaamua kusitisha ufadhili.

Marekani ilikuwa mfadhili mkubwa wa UNRWA

Marekani huchangia karibu asilimia 30 ya bajeti ya shirika hilo ambalo husaidia kutoa huduma ya afya, elimu na huduma nyingine kwa wapalestina  takriban milioni 5 katika ukanda wa Gaza, ukingo wa Magharibi, Jordan, Syria na Lebanon. Wengi wa wakimbizi hao ni watu waliovikimbia vita vya mwaka 1948 ambavyo vilipelekea kuundwa kwa taifa la Israel.

Mwanamke wa Kipalestina nje ya Shirika la UNRWAPicha: picture-alliance/dpa/M. Issa

Rais wa Marekani Donald Trump na maafisa wa utawala wake wanasema wanataka kuboresha maisha ya Wapalestina na pia kuyafufua mazungumzo ya kutafuta amani kati ya Israel na Palestina, lakini chini ya utawala wa Trump, Marekani imechukua hatua kadhaa kuwatenga Wapalestina ikiwemo kuutambua mji wa Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel, hatua ambayo imesababisha uhusiano kati ya Palestina na Israel kudorora hata zaidi.

Marekani ilichangia dola milioni 60 kwa UNRWA mwezi Januari mwaka huu, lakini ikazuia kiwango kingine cha dola milioni 65. Nabil Abu Rdainah, msemaji wa rais wa Palestina Mahmud Abbas amesema hatua za Marekani hazitafanikiwa katika kubadilisha ukweli kuwa Marekani haina tena ushawishi katika kanda hiyo na si sehemu ya kupatikana suluhisho.

Ujerumani kuongeza ufadhili

Kundi la wanamgambo la Hamas lenye makao yake katika ukanda wa Gaza pia limelaani hatua hiyo ya Marekani ya kusitisha ufadhili ikiitaja kuwa ubabe dhidi ya Wapalestina.

Watoto wa Kipalestina wakipewa mafunzo chini ya mpango wa UNRWAPicha: picture-alliance/AP Photo/H. Ammar

Serikali ya Ujerumani imeahidi kuongeza kiwango cha ufadhili wake kwa UNRWA baada ya Marekani kutangaza kustisha ufadhili.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas amesema mzozo huo wa ufadhili unachochea hali ya mashaka na kuongeza Ujerumani imeshachangia euro milioni 81 mwaka huu na inajiandaa kuongeza mchango wake.

UNRWA imekuwa ikikabiliwa na changamoto za kifedha tangu Marekani ambayo nii mfadhili wake mkubwa zaidi kupunguza mchango wake mapema mwaka huu kwa hoja kuwa shirika hilo la Umoja wa Mataifa linastahili kufanyiwa mageuzi na Wapalestina kurejea katika meza ya mazungumzo ya kutafuta amani kati yake na Israel.

Msemaji wa UNRWA Chris Gunness amesema wamesikitishwa mno na uamuzi wa Marekani wa kusitisha kabisa ufadhili lakini amepinga madai ya Marekani kuwa shirika hilo lina mapungufu makubwa katika utendaji wake.

UNRWA imesema itatafuta ufadhili zaidi kutoka kwa washirika wake Ulaya, nchi za Ghuba na Asia pamoja na kutafuta wafadhili wapya.

Mwandishi: Caro Robi

Mhariri:Isaac Gamba