Marekani yataka Iran iwajibishwe
13 Oktoba 2011Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hilary Clinton ametaka kuungwa mkono katika kuchukuwa hatua kali mpya dhidi ya Iran juu ya kwamba bado haijulikani aina ya hatua zitakazochukuliwa.
Clinton hapo jana ameyataka mataifa mengine kujiunga na Marekani katika kulaani tishio lake kwa amani ya dunia na usalama.
Amesema njama hiyo ni ukiukaji ulio dhahiri wa sheria ya kimataifa na sheria ya Marekani.
Wakati Saudi Arabia yenyewe inatafakari kuchukuwa hatua kali kutokana na kuibuka kwa njama hiyo Iran inasema hilo ni jungu lililopikwa na Marekani.
Serikali ya Iran ikijibu shutuma hizo imeishutumu Marekani kwa kutunga madai hayo ili kuondowa nadhari kwenye matatizo ya kiuchumi ya ndani ya nchi,
maandamano yanayozidi kuongezeka dhidi ya soko la hisa la Marekani la Wall Street. Baadhi ya wataalamu wanasema njama hiyo imeandaliwa na viongozi wa Iran.
Wizara ya Fedha ya Marekani imeiwekea vikwazo shirika la ndege la Mahan, shirika la ndege la kibiashara lenye makao yake mjini Tehran linalotuhumiwa kuwasafirisha kwenye eneo la Mashariki ya Kati wanachama wa Kikosi cha Kimapinduzi cha Ulinzi cha Iran wanaohusishwa na jama hiyo.
Mali za shirika hilo zimezuiliwa nchini Marekani na raia wa Marekani wamepigwa marufuku kufanya biashara na shirika hilo.
Iran imekanusha vikali kuhusika kwa njia yoyote ile kwa kile Marekani inachosema ni njama ya Kikosi cha Kimapinduzi cha Iran na Kikosi cha Quds kumuuwa balozi wa Saudi Arabia kwa kuwakodi wauwaji kutoka genge la madawa ya kulevya la Mexico kwa malipo ya dola milioni 1.5.
Rais Barack Obama wa Marekani alimpigia simu Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia kuyakinisha uhusiano wa nchi hizo mbili kwa kile Ikulu ya Marekani ilichokiita njama inayoongozwa na Iran kumuuwa balozi wa Saudi Arabia mjini Washington.
Wakitangaza habari hizo za kufadhaisha hapo Jumatatu maafisa wa serikali ya Marekani wamewataja wahusika wakuu wawili: Mansor Arbabsiar muuzaji wa magari yaliyotumika ambaye amechukuwa uraia wa Marekani na Gholam Shakuri ambaye anatajwa kuwa ni wakala wa kikosi cha Quds aliyeko Iran.
Wakati jasusi wa Marekani akijifanya kuwa mtu wa genge la madawa ya kulevya la Mexico aliyejitolea kufanya mauaji hayo amesema watu wengine wakiwemo maseneta yumkini wangeliuwawa iwapo shambulio hilo lingetekelezwa katika mkahawa mmoja.
Wakati huo huo, Saudi Arabia imelaani kile ilichokiita njama ya kuchukiza na ya kufedhesha na kwamba itaendelea na mawasiliano na Marekani juu ya suala hilo. Saudi Arabia inafikiria kuchukuwa hatua kali kukomesha vitendo hivyo vya uhalifu na kupambana vilivyo na jaribio lolote lile la kudhoofisha utulivu wa nchi hiyo ya ufalme, usalama wake na uchochezi miongoni mwa wa watu wake.
Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP/RTRE
Mhariri : Josephat Charo