1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yataka mapigano yasitishwe Yemen

3 Julai 2015

Marekani imetoa mwito mapigano Yemen yasitishwe wakati wa mwezi wa Ramadhani ili misaada ipelekwe nchini humo. Mwito huo unakuja siku moja baada ya watu wapatao 22 kuuawa na mapigano yakiendelea kuchacha mjini Aden.

Jemen Sanaa Autobombe Anschlag
Picha: Reuters/Khaled Abdullah

Marekani imetoa mwito mapigano yasitishwe Yemen wakati wa mwezi wa Ramadhani. Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani imesema katika taarifa yake kwamba kusitishwa kwa mapigano kutayaruhusu mashirika ya misaada ya kimataifa kupeleka msaada unaohitajika haraka ikiwemo chakula, dawa, na mafuta kwa raia kote nchini.

Hali ya wasiwasi imetanda kote nchini Yemen kabla sala ya Ijumaa leo kufuatia kuzuka kwa mapigano katika mji wa Aden alfajiri katika eneo la kaskazini la mji huo wa bandari ambapo waasi saba na wapiganaji watano wa serikali waliuawa. Kwa mujibu wa wakazi wa mji huo raia wawili pia waliuliwa katika mashambulizi ya makombora yaliyofanywa na waasi katika kitongoji kimoja magharibi ya Aden, na kuua raia 31 na kuwajeruhi watu zaidi ya 100.

Amin Abdullah, mkazi wa mji wa Aden, alisema, "Kilichotokea ni ufyetuliaji wa risasi kiholela wa watu wasio na hatia, wakazi, wanawake na watoto. Hivi ni vitendo vya watu waoga."

Wakati huo huo bandari iliyo karibu na kiwanda cha kusafishia mafuta cha Aden ilishambuliwa na waasi kwa siku ya tano mfululizo jana. Msemaji wa kiwanda hicho Naser al Shayef alitoa taarifa hiyo wakati mapiganao makali yalipokuwa yakiendelea katika eneo hilo.

Kiwanda cha kusafishia mafuta kilichoshambuliwaPicha: picture-alliance/dpa

Katika mkoa jirani wa Lahj na Shabwa, ndege za kivita za muungano unaoongozwa na Saudi Arabia zilifanya mashambulizi ya kutokea angani dhidi ya ngome za waasi.

Hali si shwari Sanaa

Mjini Sanaa ndege za kivita za muungano unaoongozwa na Saudi Arabia zilifanya mashambulizi 35 katika maeneo kadhaa ya waasi wa Houthi jana. Duru za madaktari zilisema waasi wanane waliuawa na wengine kumi kujeruhiwa katika mashambulizi hayo, waliyoyaeleza kuwa mabaya kabisa tangu kuanza kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani wiki mbili zilizopita.

Mashambulizi hayo pia yaliyalenga makazi ya jenerali wa zamani wa jeshi, Ali al Kahlani, lakini wakazi walisema hakuna aliyeumia. Mlinzi wa jenerali huyo, Abu Asil al Ziyadi, alisema, "Mwendo wa saa tano mchana kulifanyika shambulizi la kinyama katika makazi ya meja jenerali Ali Mohammed Al Kahlani kutumia makombora mawili. Uharibifu uliotokea kwa majirani ulitokana na shambulizi hilo lakini tunamshukuru Mungu hakuna aliyekufa."

Muungano huo umekuwa ukiwashambulia waasi hao wanaoungwa mkono na Iran na washirika wake tangu tarehe 26 mwezi Machi mwaka huu kumuunga mkono rais wa Yemen, Abedrabbo Mansour Hadi, aliyekimbilia Saudi Arabia.

Bomu lililokuwa limetegwa kwenye gari limelipuka karibu na msikiti mmoja mjini Sanaa lakini hakukutolewa taarifa kuhusu waliokufa au kujeruhiwa katika hujuma hiyo ya jana.

Shambulizi la bomu lililotegwa kwenye gari SanaaPicha: picture-alliance/dpa/Y. Arhab

Machafuko ya Yemen yalitokea siku moja tu baada ya Umoja wa Mataifa kutangaza hali ya dharura ya kibinaadamu nchini humo, ambako watu kiasi ya 3,000 wameuliwa tangu mwezi Machi mwaka huu, nusu yao wakiwa raia. Yametokea pia baada ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO, kutangaza kwamba miji miwili ya kale nchini humo iliyo katika orodha yake ya turathi za kimataifa iko hatarini kutokana na machafuko hayo.

Shirika la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International lilionya kuhusu hasara kubwa wanayoendelea kuipata raia wakati wa mashambulizi ya kutokea angani yanayofanywa nchini kote na kuushutumu muungano unaoongozwa na Saudi Arabia huo kwa kushindwa kuheshimu sheria za kimataifa.

Mwandishi:Josephat Charo/AFP/RTRE

Mhariri:Abdu Mtullya