1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Marekani yataka msaada kulinda ujia wa Hormuz, EU yakataa

17 Machi 2026

Wakati Trump akiongeza shinikizo kwa Ulaya kulinda Ujia wa Hormuz, Urusi inanufaika na kupanda kwa bei ya nishati jambo linaloiathiri Ukraine na washirika wake wa Ulaya.

Umoja wa Falme za Kiarabu, Dubai 2026 | Meli za biashara zikiwa nje ya pwani wakati wa vita vya Iran
Hatua ya Iran kuuzuia Mlango-Bahari wa Hormuz imeutumbukiza uchumi wa dunia katika mgogoroPicha: AFP/Getty Images

Rais wa Marekani Donald Trump kuitaka Ulaya kusaidia kulinda njia ya usafirishaji wa meli za mafuta na gesi katika Mlango wa Hormuz ilikuwa mada kuu katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya uliofanyika Jumanne mjini Brussels.

Baadhi ya nchi wanachama ziliashiria kuwa hazitaki NATO ihusishwe katika kulinda mlango huo, ambao umefungwa kwa sehemu kubwa na Iran kufuatia mashambulizi ya mabomu ya pamoja ya Marekani na Israel.

Wazungu hawako tayari kupeleka wanajeshi kulinda Mlango wa Hormuz "kwa sababu hatua hiyo ingewafanya kuwa shabaha inayoweza kushambuliwa na Iran,” anasema Charles Hecker kutoka Taasisi ya Royal United Services Institute (RUSI) akizungumza na DW.

Mwanzoni mwa mkutano huo wa Jumatatu, mwanadiplomasia mkuu wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas alisema ni kwa manufaa ya kanda hiyo kuhakikisha Mlango wa Hormuz unabaki wazi, na kwamba wanajadili hatua wanazoweza kuchukua kutoka upande wa Ulaya.

Aliongeza kuwa Umoja wa Ulaya unaendelea kuwasiliana na "wenzetu wa Marekani katika ngazi mbalimbali.”

Hata hivyo, mwishoni mwa mkutano alisema hakuna "hamu” miongoni mwa nchi wanachama kutanua operesheni ya kijeshi ya baharini ya Umoja wa Ulaya hadi Mlango wa Hormuz kwa sasa.

Kupanda kwa bei ya nishati barani Ulaya na mizozo ya nishati inayofuata kumeongeza mvutano katika uhusiano uliokuwa tayari umeathirika kati ya Ulaya na Marekani.

Mawaziri wa Umoja wa Ulaya pia walitathmini namna mzozo huo unavyoweza kuipa Urusi nafasi ya kupata nguvu zaidi, kwa kutumia mapato ya ziada kutoka mauzo ya nishati kufadhili vita vyake nchini Ukraine.

"Mshindi pekee wa kweli katika vita dhidi ya Iran kwa sasa ni Urusi,” alisema Hecker.

Iran inavyoweza kujilinda dhidi ya mashambulizi ya Marekani

01:42

This browser does not support the video element.

Trump aongeza shinikizo kwa Ulaya

Jumapili, Trump aliongeza shinikizo kwa nchi zinazopokea nishati kupitia Mlango wa Hormuz kuhakikisha usalama wa njia hiyo ya maji, ambayo kwa kawaida hupitisha takriban asilimia 20 ya mafuta ghafi ya dunia.

Ingawa wanunuzi wakuu wa shehena hizo ni mataifa ya Asia, Trump ameonekana tena kuutishia muungano wa NATO.

"Ni sahihi kwamba wanaonufaika na mlango huo wasaidie kuhakikisha hakuna jambo baya linalotokea,” alisema katika mahojiano na gazeti la Financial Times. "Kama hakutakuwa na mwitikio au kutakuwa na majibu hasi, nadhani hilo litakuwa baya kwa mustakabali wa NATO.”

Hecker alisema hii ni juhudi ya Trump kuwashawishi Wazungu kujihusisha zaidi katika vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

Alisema bado haijulikani ni aina gani ya tishio analolitoa Trump kwa NATO au angewezaje kulitekeleza, lakini anajaribu kutumia shinikizo kwa nchi anazotaka ziingie katika mzozo huo.

Trump amezitaka hasa Ufaransa na Uingereza kujiunga na juhudi hizo, lakini Hecker alisema ni vigumu kwa nchi hizo kuhusika wakati mapigano bado yanaendelea.

Aliongeza kuwa haziko tayari kujiunga na operesheni za kijeshi za Marekani katika Mlango wa Hormuz kwa siku za usoni, si tu kwa sababu zingekuwa malengo ya Iran, bali pia kwa sababu hazielewi wazi malengo na mkakati wa Marekani na Israel katika vita hivyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Johann Wadephul alisema haoni nafasi ya NATO katika kulinda mlango huo na alitarajia Ulaya kupewa taarifa na Marekani na Israel kuhusu malengo na mipango yao.

Alisema haoni kuwa NATO imefanya uamuzi wowote kuhusu suala hilo au inaweza kuchukua jukumu la kulinda Mlango wa Hormuz.

Hata hivyo, Ufaransa imeonyesha msimamo wenye unafuu zaidi. Rais Emmanuel Macron alisema nchi yake iko tayari kusaidia kulinda mlango huo mara tu awamu kali ya mzozo itakapopungua.

Wakati mataifa ya Ghuba yenye utajiri wa mafuta na gesi yakishambuliwa na Iran, hofu ya upungufu wa usambazaji imeongezekaPicha: John Moore/picture alliance/AP Photo

Ulaya yaathiriwa na kupanda kwa bei ya nishati

Umoja wa Ulaya tayari unakabiliwa na athari za kiuchumi kutokana na mzingiro huo. Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen alisema tangu kuanza kwa mzozo, bei ya gesi imeongezeka kwa asilimia 50 na bei ya mafuta kwa asilimia 27.

Alilieleza Bunge la Ulaya kuwa katika siku 10 tu za vita dhidi ya Iran, walipa kodi wa Ulaya wamelipa euro bilioni 3 zaidi kwa uagizaji wa mafuta na gesi.

Aliongeza kuwa Ulaya si mzalishaji wa mafuta wala gesi, hivyo inategemea uagizaji wa gharama kubwa na wenye hatari ya mabadiliko ya bei, jambo linaloiweka katika hali ngumu ikilinganishwa na maeneo mengine.

Ili kupunguza bei, nchi za Ulaya zikiwemo Ufaransa, Ujerumani, Italia na Uingereza ziliunga mkono uamuzi wa kutoa mamilioni ya mapipa ya mafuta kutoka akiba za dharura pamoja na wanachama wengine wa kundi la G7. Wakala wa Kimataifa wa Nishati umetaka mapipa milioni 400 ya mafuta yawekwe sokoni.

Ingawa von der Leyen alionya dhidi ya kurejea sera ya kununua nishati kutoka Urusi, Umoja wa Ulaya unatambua kuwa vita dhidi ya Iran vinaipa Urusi mapato makubwa ya ziada.

Je, Urusi inanufaika zaidi?

Wakati Iran ilipolenga hoteli, viwanja vya ndege na hata mitambo ya kusafisha mafuta katika Ghuba na kuzuia Mlango wa Hormuz, Urusi ilikuwa tayari kutumia fursa hiyo.

Bei ya mafuta ilipofikia euro 87.20 — kiwango cha juu zaidi tangu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mwaka 2022 — Moscow ilianza kuwasilisha rasilimali zake za nishati kama mbadala kwa wanunuzi waliokuwa na uhitaji mkubwa.

Msemaji wa Rais Vladimir Putin, Dmitry Peskov, alisema Urusi imekuwa na itaendelea kuwa msambazaji wa kuaminika wa mafuta na gesi, huku mshauri wa Kremlin Kirill Dmitriev akikosoa uamuzi wa Ulaya kuachana na nishati ya Urusi.

Ili kudhibiti kupanda kwa bei, Trump aliondoa kwa muda baadhi ya vikwazo vya ununuzi wa mafuta ya Urusi, ikiwa ni pamoja na kutoa msamaha wa siku 30 kwa India.

Je, Afrika ina kinga dhidi ya bei ya mafuta kupanda duniani?

04:26

This browser does not support the video element.

Wazungu wana hofu kuwa kupanda kwa bei ya nishati kutaongeza mapato ya Urusi na kuiwezesha kuendelea au hata kuongeza nguvu katika vita dhidi ya Ukraine.

Wasiwasi mwingine ni kwamba vifaa muhimu vya ulinzi vinavyohitajika Ukraine, kama makombora ya Patriot ambayo Ulaya hununua kutoka Marekani, vinaweza kuelekezwa sasa katika eneo la Ghuba.

Kaja Kallas alibainisha kuwa vita dhidi ya Iran vina athari ya moja kwa moja kwa Ukraine, kwani uwezo wa ulinzi unaohitajika huko sasa unaelekezwa Mashariki ya Kati.

Kwa mujibu wa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy, nchi za Ghuba zimetumia makombora ya Patriot mengi zaidi katika siku chache za mashambulizi ya Iran kuliko Ukraine ilivyotumia tangu kushambuliwa na Urusi miaka minne iliyopita.

Ukraine imezipa nchi za Ghuba teknolojia yake ya kukabiliana na droni kwa matumaini kwamba zitatumia mifumo hiyo ya ndani na kuhifadhi makombora ya Patriot kwa mashambulizi ya makombora pekee.

Mchambuzi Rafael Loss wa Baraza la Ulaya la Mahusiano ya Kigeni alisema Ukraine ina uzoefu wa miaka kadhaa wa kudungua droni za aina ya Shahed zinazotumiwa na Iran, na imeunda mifumo madhubuti ya kukabiliana nazo ambayo sasa inatoa kwa nchi za Ghuba.

Lengo ni kupunguza mahitaji ya makombora ya Patriot katika eneo la Ghuba ili Ukraine iweze kupata zaidi katika siku zijazo, alisema Loss.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW