Marekani yatakiwa kutafakari upya uamuzi wake kuhusu WHO
31 Mei 2020Serikali ya Trump imesema imesimamisha ufadhili huo kutokana na jinsi WHO ilivyolishughulikia janga la virusi vya corona, ambalo limesababisha vifo vya zaidi ya watu 366,000 na pia kuuharibu uchumi wa dunia. Trump amedai kuwa WHO inadhibitiwa na China.
Marekani ndio iliyokuwa mfadhili mkubwa wa shirika hilo na kujiondoa kwake kutaliathiri pakubwa shirika la afya duniani. Mwaka uliopita Marekani ilitoa mchango wake wa dola milioni 400 kwa shirika hilo la afya la kimataifa.
Umoja wa Ulaya umeihimiza Marekani kutafakari upya uamuzi wake huo wa kuondoa kabisa ufadhili kwa shirika la afya duniani WHO. Katika taarifa iliyotolewa kwa pamoja na, Rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula Von der Leyen na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja huo Josep Borell, viongozi hao wamesema wakati ambapo ulimwengu unakabiliwa na kitisho cha janga la maambukizi ya virusi vya corona, dunia inapaswa kuimarisha ushirikiano na kutafuta suluhuhisho kwa pamojaViongozi hao wa Umoja wa Ulaya wamesisitiza kwamba vitendo vinavyodhoofisha juhudi za kimataifa za kutafuta matokeo mazuri vinapaswa kuepukwa na kila upande. Ursula von der Leyen anamesema Umoja wa Ulaya tayari umeongeza fedha za ufadhili kwa shirika la afya. Amesema kwa WHO, kushughulikia mahitaji ya dharura ya afya duniani unahitajika ushirikiano na misaada kutoka kwa wahusika wote. Waziri wa Afya wa Ujerumani, Jens Spahn amesema uamuzi huo wa rais Trump unarudisha nyuma maendeleo katika sekta ya afya ulimwenguni kote.
Lawrence Gostin, profesa wa sheria ya afya ya duniani katika Chuo Kikuu cha Georgetown na mshirika wa WHO, amehoji uwezo wa Trump kujiondoa kutoka kwenye shirika hilo kwa kujiamulia mwenyewe bila idhini ya bunge, amesema hatua hiyo si halali, haina maana na ni hatari.
Wakati hayo yakiendelea nchi nyingi zinakabiliwa na shinikizo ikiwa ni pamoja na maandamano ya kudai kuondolewa hatua za karantini licha ya wataalam wa afya kutahadharisha kutokea kwa wimbi la pili la maambukizi ya virusi vya corona iwapo watu watarejea haraka kwenye hekaheka zao za kila siku.
Kwa mujibu wa Chuo kikuu cha Johns Hopkins watu 960 wamefariki kutokana na COVID -19 nchini Marekani katika kipindi cha saa 24 zilizopita. Hadi sasa Marekani imethibitisha jumla ya watu 1,769,776 walioambukizwa virusi vya corona ikiwa ndio inaongoza ulimwenguni.
Chanzo:/AFP