Marekani yatangaza kitita kipya cha msaada kwa Ukraine
15 Mei 2024Marekani imetangaza leo msaada wa kijeshi wa nyongeza kwa Ukraine wenye thamani ya dola bilioni 2 kuvisaidia vikosi vya nchi hiyo kupambana na wanajeshi wa Urusi wanaosonga mbele kwa kasi katika eneo la mstari wa mbele wa vita.
Soma: Blinken: Msaada wa kijeshi kwa Ukraine utawasili hivi karibuni
Tangazo la msaada huo limetolewa na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken mwishoni mwa ziara yake mjini Kyiv iliyoanza jana. Amesema msaada huo wa nyongeza unanuwia kupeleka silaha haraka kwa vikosi vilivyo uwanja wa mapambano na kulisaidia taifa hilo kununua zana zaidi za kijeshi.
"Tunaharakisha kupeleka risasi, magari ya kijeshi, makombora, mifumo ya ulinzi wa anga, ili vifike kwenye uwanja wa mapambano kuwalinda wanajeshi na raia. Na kuhusu mifumo ya ulinzi wa anga, hicho ni ndiyo kipaumbele chetu cha juu".
Msaada huo unatolewa katikati ya mashambulizi makali ya Urusi yaliyovilazimisha vikosi vya Ukraine kurudi nyuma kutoka vijiji kadhaa vya mkoa wa Kharkiv.