1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Marekani yatangaza msaada mpya kwa Ukraine

13 Desemba 2024

Serikali ya Rais wa Marekani Joe Biden, imetangaza msaada mwingine wa silaha kwa Ukraine wa thamani ya dola milioni 500.

Marekani iliahidi kuendelea kutoa misaada zaidi kwa Ukraine hadi mwisho wa utawala wa Rais Joe Biden.
Marekani iliahidi kuendelea kutoa misaada zaidi kwa Ukraine hadi mwisho wa utawala wa Rais Joe Biden.Picha: Kento Nara/Geisler-Fotopress/picture alliance

Hayo ni kwa mujibu wa waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Antony Blinken.

Katika taarifa, Blinken amesema msaada huo unajumuisha risasi za mfumo wa hali ya juu wa maroketi wa HIMARS na makombora ya Kasi ya Kuzuia mionzi (HARMs) miongoni mwa misaada mingine.

Awali, msemaji wa Ikulu ya Marekani John Kirby alisema nchi hiyo itaendelea kutoa misaada zaidi kwa Ukraine hadi mwisho wa utawala wa Biden.

Siku 10 zilizopita, Marekani ilisema itapeleka nchini Ukraine makombora, risasi, na silaha nyingine za thamani ya dola milioni 725.

Utawala wa Biden unaomaliza muda wake, unatafuta kuiimarisha Ukraine katika mapambano yake dhidi ya Urusi, kabla ya rais mteule wa nchi hiyo Donald Trump kuchukuwa rasmi madaraka mnamo mwezi Januari.

Ukraine yaomba kupewa mifumo zaidi ya ulinzi wa anga

Katika tukio jingine Ukraine imetangaza kuwa imekuwa ikipambana kuzuia mashambulizi mapya ya makombora kwenye miundombinu yake ya nishati, ambayo ni ya hivi punde zaidi katika kampeni ya Urusi inayolenga gridi ya umeme ya nchi hiyo iliyoharibiwa na vita.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Andrii Sybiha amewatolea wito washirika wa Kiev kuwasilisha haraka mifumo zaidi ya ulinzi wa anga ili kuzuia vitendo hivyo vya ugaidi. 

Urusi imezidisha mashambulizi yake kwenye miundombinu ya nishati ya Ukraine, na hivyo kupelekea mamia kwa maelfu ya watu kukosa umeme na kushindwa kupasha joto majumba yao katika msimu huu wa baridi kali.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW