1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yatangaza sheria mpya dhidi ya wahamiaji

22 Februari 2017

Wizara ya usalama wa ndani ya Marekani imetangaza sheria mpya zitakazowalenga wahamiaji wasiokuwa na vibali. Inakadiriwa kuwa kuna watu milioni 11 nchini humo wasiokuwa na vibali.

USA Republikaner Donald Trump in Green Bay Wisconsin
Picha: Getty Images/D. Hauck

Utawala wa rais wa Marekani Donald Trump, umetangaza amri mpya juu ya wahamiaji haramu.Sheria hizo kali zinalenga kuwaandama  wageni wanaoshi nchini humo bila vibali rasmi, hatua ambayo itawaweka matatani watu milioni 11 wanaoishi nchini humo bila vibali.

Amri hizo zimeibua wasiwasi mwingi miongoni mwa mamilioni ya jamii ya wahamiaji, ambao kwa miaka mingi wameishi nchini humo wakikuza jamii zao na kuendeleza maisha. Lakini kwa mara ya kwanza baada ya miongo mingi, watu hao ambao wengi wao wanatokea Mexico na America ya kati sasa wameingiwa na khofu kutokana na uwezekano wa kufurushwa.

Sheria hizo mpya zitawawezesha maafisa wanaoshika doria katika mipaka na maafisa wa uhamiaji kumfurusha mhamiaji yeyote asiyekuwa na kibali.

Sheria hizo hazitawalinda baadhi ya watu jinsi ilivyokuwa katika utawala wa Barrack Obama, bali wote wanaokiuka sheria wanaweza kulengwa kwenye mchakato wa kufurushwa. Kadhalika wazazi ambao walitumia wanaofanya biashara ya kuwaingiza watu kimagendo nchini Marekani kuingiza watoto wao pia wanaweza Kukabiliwa na sheria.

Waziri wa mambo ya ndani anayehusika na usalama John Kelly, amesema amri hizo ni muhimu katika kukabiliana na matatizo aliyosema yamepindukia uwezo wa rasilmali za serikali.

Maafisa na mawakala wa mpakani katika kituo cha San Ysidro, CaliforniaPicha: Getty Images/AFP/S. Huffaker

Sean Spicer ambaye ni msemaji wa Ikulu amesema sheria hizo zinaeleza mikakati na sera za kuimarisha usalama kulingana na sheria za uhamiaji. "Ilani kuhusu amri ya usalama wa mipaka na uimarishaji wa sheria za uhamiaji zinaleza hatua ambazo wizara ya usalama izachukua kulinda mipaka ya kusini mwa nchi, kuzuia uingiaji zaidi wa wahamiaji na kuwarudisha makwao wahamiaji wasiokuwa na vibali kwa njia ya kibinadamu."

Pingamizi dhidi ya amri hizo

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yametaja hatua hiyo kama uonevu na kuonya kuwa kuwafurusha watu wengi kutaathiri familia ambazo mizizi yao imejikita nchini Marekani. Halikadhalika kutaathiri uchumi wa nchi hiyo.

Seneta Ben Cardin wa chama cha Democrats ameonya kuwa sheria hizo zitaathiri usalama wan chi na umma, huku Meya wa New York Bill De Blasio akisema hawezi kuwageuza maafisa wa polisi wa jiji kuwa mawakala wa uhamiaji wala kuiunga mkono sera ambayo mwisho wake itaathiri umoja ambao umesaidia kukuza usalama wa jiji hilo.

Ili kufanikisha juhudi hizo, serikali itawaajiri maafisa 10,000 wa uhamiaji na mawakala 5,000 kushika doria mipakani. Sheria hizo ni kulingana na amri za Rais Donald Trump punde tu baada ya kuapishwa kuwa rais, kwamba maafisa waimarishe usalama na wawakabili wahamiaji wasiokuwa na vibali na kuamuru kujengwa ukuta kati ya Marekani na Mexico. Katika sheria hizo, waziri Kelly ameamuru kuwa mipango ya kujengwa kwa ukuta ianze.

Hatua hii inajiri kabla rais wa Mexico Enrique Pena Nieto kukutana na waziri wa nchi za nje wa Marekani Rex Tillerson na mwenzake wa mambo ya ndani John Kelly.

Mwandishi: John Juma/AFPE/DPE

Mhariri: Yusuf Saumu

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW