1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Marekani yatangaza vikwazo vipya 500 dhidi ya Urusi

Josephat Charo
24 Februari 2024

Rais wa Marekani Joe Biden ametangaza vikwazo vipya 500 dhidi ya Urusi Ijumaa (23.02.2024) ikiwa ni mwaka wa pili tangu Urusi ilipoivamia Ukraine.

USA | Rede Präsident Joe Biden zum Ukraine-Israel-Hilfspaket
Joe Biden, rais wa MarekaniPicha: Evan Vucci/AP Photo/picture alliance

Katika taarifa rais wa Marekani Joe Biden amesema ikiwa Putin hatalipa kwa vifo na uharibifu, ataendelea na gharama kwa Marekani pamoja na washirika wake wa jumuiya ya kujihami ya NATO, Ulaya na kote ulimwenguni itaongezeka.

Balozi wa Urusi nchini Marekani Anatoly Antonov amesema vikwazo hivyo ni jaribio linalojali masilahi binafsi na linalopuuzilia mbali maadili yanayokubalika kwa lengo la kuingilia mambo ya ndani ya shirikisho la Urusi.

Vikwazo hivyo vinavyoelezwa kuwa hatua kubwa ya pamoja kuwahi kuchukuliwa tangu kuanza kwa vita, pia inapania kuweka gharama kwa kifo cha wiki iliyopita cha mkosoaji mkali ya rais Putin,Alexei Navalny katika gereza la Siberia, huku hatua zikichukuliwa dhidi ya maafisa watatu.

Hata hivyo vikwazo hivyo havikwenda mbali kuchukua hatua madhubuti za kuleta mabadiliko kama vile kuifadhili Ukraine kwa kuzuia mali za Urusi, ambayo uchumi wake umeendelea kukua licha ya miaka miwili ya shinikizo.

Jitihada mpya ya kiuchumi inakuja wakati Urusi ikipiga hatua za kwanza za mafanikio katika kipindi cha miezi kadhaa katika uwanja wa vita nchini Ukraine, ambayo imelazimika kutumia risasi kwa uangalifu kutokana na uhaba kwa sababu ya mkwamo wa kisiasa mjini Washington ukikwamisha msaada mpya wa kijeshi kutoka kwa Marekani.

Akizungumza siku moja kabla kutimia miaka miwili tangu vita vya Ukraine vilipoanza, Biden alisema: "Hatuwezi kukimbia sasa."

Soma pia: Kifo cha Navalny pigo kwa upinzani nchini Urusi

Vikwazo vipya vinaulenga mfumo wa kadi ya mkopo ya Mir, iliyoanzishwa na Urusi kuepuka kuitegemea mifumo ya Marekani. Wizara ya fedha ya Marekani pia ilisema inazilenga fedha za uwekezaji na mabenki ya kikanda kuilenga miundombinu ya msingi ya kifedha ya Urusi.

Naibu waziri wa fedha wa Marekani Wally Adeyemo alisema serikali ya mjini Washington inafanya kazi kwa bidii na washirika wake kuzingatia njia za kuisaidia Ukraine. "Kimsingi, hatutafanya kitu chochote kwa mali za Urusi mpaka tutakaposonga mbele kama muungano," Adeyemo aliwaambia waandishi wa habari.

Rais wa Urusi, Vladimir Putin, kulia.Picha: Alexander Kazakov/Sputnik, Kremlin Pool Photo/AP/picture alliance

Awali muungano unaozijumuisha nchi saba zilizostawi kiviwanda za G7, Umoja wa Ulaya na Australia zilitangaza mipango ya kuimarisha utekelezaji wa vikwazo hivyo kwa kuweka bei ya dola 60 kwa kila pipa la mafuta ghafi la Urusi, ambayo imekuwa ikikwepwa.

Biashara muhimu za Urusi zalengwa na vikwazo

Biashara muhimu zilizolengwa ni pamoja na kampuni ya usafiri ya Urusi JSC SUEK, ambayo inatajwa kutoa huduma kwa wizara ya ulinzi ya Urusi, na hususan kampuni ya kutengeneza chuma cha pua ya Mechel.

Kampuni nyingine ni ya uchapishaji wa mfumo wa 3D, vilainishi, roboti na mbinu ya kufanya kifaa, mchakato au mifumo ifanye kazi yenyewe bila kuendeshwa na mtu.

"Vikwazo vitahakikisha rais Putin analipa gharama kubwa zaidi kwa uvamizi wake mpana na ukandamizaji nyumbani," alisema Biden katika taarifa. Biden pia alisema, "Tunaziwekea vikwazo kampuni karibu 100 kwa kutoa msaada kwa mlango wa nyuma kwa mfumo wa vita wa Urusi."

Biden pia alitangaza kwamba anamchukulia rais wa Urusi Vladimir Putin kuwa na dhamana kwa kifo cha Navalny, ambaye aliponea chupu chupu shambulizi la sumu 2020 ambalo aliwalaumu mawakala wa serikali.

Vikwazo hivyo dhidi ya maafisa watatu kutokana na kifo cha Navalny vinafuatia hatua kama hiyo iliyochukuliwa na Uingereza. Baadhi ya serikali za nchi za Ulaya pia ziliwaita mabalozi wa Urusi kuwasilisha malalamiko yao.

Siku ya Ijumaa ikulu ya Marekani ilisema serikali ya mjini Washington itachukua hatua zaidi kufuatia kifo cha Navalny, ikisema vikwazo vipya ni mwanzo tu.

Katika kutangaza vikwazo hivyo, rais Biden alitoa wito mpya kwa bunge la Marekani lipitishe msaada wa kijeshi kwa Ukraine. Spika wa bunge wa chama cha Republican Mike Johnson amekataa kuuwasilisha muswada wa msaada kwa ajili ya Ukraine upigiwe kura bungeni, huku mshirika wake, rais wa zamani Donald Trump, akiukosoa msaada kwa ajili ya serikali ya mjini Kyiv.

"Historia inatazama, saa inasonga, wanajeshi na raia jasiri wa Ukraine wanakufa," Biden alisema Ijumaa, akihimiza muswada huo upitishwe.

(afpe, ape)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW