1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yatatua mgogoro wa bajeti

Abdu Said Mtullya2 Januari 2013

Baada ya mvutano wa miezi kadhaa wabunge wa Marekani wamefikia mwafaka juu ya mgogoro wa bajeti. Mswada uliopitishwa na wabunge hao umeepusha kinachoitwa kuzungumkuti cha bajeti

Rais Barack Obama na Makamu wake Joe Biden baada ya wabunge kupiga kura
Rais Barack Obama na Makamu wake Joe Biden baada ya wabunge kupiga kuraPicha: Reuters

Rais Barack Obama amesema juhudi za kuubadilisha mfumo wa kodi unaowapendelea matajiri zimefanikiwa. Rais Obama amesema hayo baada ya Baraza la wawakilishi kuupitisha mswada wa kuiepusha Marekani na mgogoro wa kiuchumi.

Akizungumza baada ya wabunge kuupitisha mswada huo Rais Obama alisema kuwa kura za wabunge zimeuepusha mchanganyiko wa kupandisha kodi mara moja, na kukata matumizi ya mfuko wa kijamii, mchanganyiko ambao ungeliirudisha Marekani katika mshuko mwingine wa uchumi. Hata hivyo amekiri kwamba nakisi katika bajeti ya Marekani bado ni kubwa sana.

Obama ameeleza kwamba Marekani bado inawekeza kidogo kwa ajili ya yale yanayohitajika kufanyika ili kuustawisha uchumi haraka. Amesema Wamerakani hawawezi kutumia njia ya mkato ili kufikia kwenye neema .

Obama ameeleza kuwa anakubaliana na wajumbe wa Republican na Democrats kwamba nakisi lazima ipunguzwe. Lakini amesema kupunguza nakisi lazima kuende sambambana mageuzi katika mfumo wa kodi. Amesisitiza kuwa ni lazima Marekani isonge mbele katika kupunguza nakisi, lakini kwa wizani"

Rais Barack Obama akihutubia BungePicha: Reuters

Rais Obama aliekatiza mapumziko yake huko Hawaii ili kurejea Washington kuhimiza kufikiwa kwa suluhisho la bajeti atautia saini mswada huo ili uwe sheria. Lakini amesisitiza kuwa harakati za kupambana na nakisi zitaendelea.

Deni la Marekani limekuwa linaongezeka katika kipindi cha miaka10 iliyopita na kufikia dola Trilioni 16 sasa. Sababu kadhaa zimeisababisha nakisi hiyo kubwa, ikiwa pamoja na, hatua iliyochukuliwa na utawala wa George Bush ya kupunguza kodi. Vita vya Iraq na Afghanistan, mshuko wa uchumi na mgogoro wa fedha pia ni sababu zilizochangia katika kuiongeza nakisi hiyo.

Mswada uliopendekezwa na Seneti na kuridhiwa na Baraza la wawakilishi utazuia kupandishwa kodi kwa Wamarekani wote na utaepusha kukatwa kwa mfuko wa matumizi. Badala yake kodi zitapandishwa kwa familia zenye mapato yanayovuka dola laki nne kwa mwaka. Kodi kwa familia hizo zitapanda kwa asilimia 39.6 kutoka kiwango cha sasa cha asilimia 35. Kupandishwa kodi kwa familia hizo kutaingiza mapato ya dola Bilioni 620 katika kipindi cha miaka kumi ijayo. Mswada huo pia utawezesha kuurefusha kwa mwaka mmoja, muda wa kuwalipa Wamarekani milioni mbili wasiokuwa na ajira.

Hatua ya kukata matumizi itaahirishwa kwa muda wa miezi miwili wakati bunge linatafakari mpango mbadala. Wabunge 257 walipiga kura ya ndio kuipitisha rasimu hiyo na167 waliipinga. Kura zilipigwa saa 24 tu baada ya Seneti kuipitisha rasimu hiyo ambapo masenata 89 waliiunga mkono na wengine wanane waliipinga.

Mwandishi:Müller Sabine
Tafsiri:Mtullya abdu.
Mhariri: Gakuba Daniel