1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yatetea uamuzi wa Israel kuitambua Somaliland UN

Amina Abubakar afp, reuters
30 Desemba 2025

Marekani imetetea haki ya Israel ya kuitambua Somaliland kama dola huru katika Umoja wa Mataifa, ikisema uamuzi huo ni sawa na namna Palestina ilivyotambuliwa kuwa dola huru na nchi kadhaa duniani.

Tammy Bruce
Naibu balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Tammy BrucePicha: Celal Gunes/picture alliance/Anadolu

Tammy Bruce, naibu balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa aliuambia mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja huo kwamba, Israeli ina haki sawa ya kuwa na mahusiano ya kidiplomasia kama ilivyo kwa nchi nyingine yoyote huru.

Aliendelea kusema kwamba mapema mwaka huu, nchi kadhaa zikiwemo nchi wanachama wa Baraza hilo, zilifanya uamuzi wa pamoja wa kuitambua Palestina kama dola, akisisitiza kuwa baada ya uamuzi huo hakuna mkutano wowote wa dharura ulioitishwa na Baraza hilo  kukemea uamuzi huo, huku akilitumuhu Baraza hilo kuwa na undumilakuwili.

Kauli ya Tammy Bruce imetokana na ukosoaji mkubwa unaoendelea baada ya Israel kutangaza kuitambua Somaliland kama dola huru,  tamko lililokosolewa vikali na Umoja wa Afrika, Misri na Umoja wa Ulaya. Hata hivyo rais wa Marekani Donald Trump alisema anapinga Somaliland kutambuliwa kama dola huru na Bruce alisema hivi karibuni kwamba hapajakuwa na mabadiliko yoyote katika sera ya Marekani.

Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud Picha: Odd Andersen/AFP/Getty Images

Balozi wa Slovenia, Samuel Zbogar, ambaye nchi yake iliitambua Palestina, alikanusha sababu zilizotolewa na Marekani kuhusu hatua iliyochukuliwa na israel kuhusu Somaliland. "Palestina si sehemu ya nchi yoyote. Ni eneo lililokaliwa kinyume cha sheria, kama ilivyotangazwa na Mahakama ya Kimataifa ya Haki, wakati Somaliland ikiwa sehemu ya nchi mwanachama wa UN na kuitambua kunakwenda kinyume na Mkataba wa Umoja wa Mataifa,” alisema Zbogar.

Somalia yakosoa tamko la Israel

Kama mmoja wa wanachama wa hivi karibuni wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, balozi wa Somalia Abukar Osman alikosoa uamuzi wa Israel kuitambua Somalilanda kama dola huru.  Osman amesema uichokozi wa aina hiyo unalenga kuisambaratisha Somalia akitoa wito kwa Umoja huo kuukataa uamuzi huo.

Nchi kadhaa wanachama zilionyesha kuiunga mkono Somalia bila kuitaja Israel. Balozi wa Uingereza James Kariuki ameahidi kwamba nchi yake inaunga mkono uhuru wa somalia, uhuru wa kisiasa na umoja wa  taifa hilo. Nae muakilishi wa Israeli Jonathan Miller alisema hatua iliyochukuliwa sio ya uhasama dhidi ya Somalia, na haizuii mazungumzo ya siku za usoni kati ya pande husikabali ni ya kuimarisha uthabiti wa eneo hilo.

Somaliland ilijitenga na kutangaza uhuru wake kutoka Somalia mwaka 1991 na imekuwa ikitafuta bila mafanikio utambuzi wa kimataifa hadi tangazo la hivi karibuni la  Israeli la kuitambua rasmi kama dola huru.

Somaliland iliyopo katika Pembe ya Afrika, eneo lake la Kaskazini linapakana na Ghuba ya Aden kutoka Yemen, na kuifanya iwe muhimu katika masuala ya kimkakati.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW