1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yathibitisha kifo cha kiongozi wa al Shabaab

6 Septemba 2014

Wizara ya ulinzi ya Marekani jana Ijumaa(05.09.2014)imethibitisha kuwa Ahmed Abdi Godane, kiongozi wa kundi la al-Shabaab, ameuwawa katika shambulio la anga la Marekani nchini Somalia wiki hii.

Kämpfer von Al-Shabaab in Somalia
Wapiganaji wa al Shabaab nchini SomaliaPicha: picture-alliance/AP Photo/F.-A.Warsameh

Wizara ya ulinzi ya Marekani imesema kuwa hilo ni pigo kubwa kwa kundi hilo lenye mafungamano na al-Qaeda.

"Tumethibitisha kwamba Ahmed Godane, muasisi mwenza wa al-Shabaab , ameuwawa," Admirali John Kirby, msemaji mkuu wa wizara ya ulinzi , amesema katika taarifa.

Ahmed Abdi Godane kiongozi wa al Shabaab aliyeuwawaPicha: Rewards for Justice/AFPGetty Images

tangu kuchukua madaraka ya kundi la al-Shabaab mwaka 2008, Godane ameliunda upya kundi hilo na kuwa mhusika mkubwa duniani katika mtandao wa al-Qaeda, akifanya mashambulio ya mabomu na mashambulizi ya kujitoa muhanga nchini Somalia na kwengineko katika kanda hiyo, ikiwa ni pamoja na shambulio la Septemba 21, mwaka 2013 katika jengo la maduka la Westgate mjini Nairobi, Kenya ambapo watu 67 waliuwawa.

Godane alidai hadharani kuhusika na shambulio la Westgate, akisema ni kulipiza kisasi kwa Kenya na mataifa ya magharibi kujihusisha ndani ya Somalia na kudokeza kuhusiana na kuwapo karibu na kumbukumbu ya shambulio la Septemba 11, mwaka 2001 nchini Marekani.

Kifo chake kinaacha pengo katika uongozi wa kundi la al-Shabaab na kinaonekana kutoa changamoto kubwa kwa umoja wa kundi hilo tangu kujitokeza kama nguvu kuu ya mapambano ya miaka nane iliyopita.

Jengo lililoporomoka la Westgate mjini NairobiPicha: DW/A. Kiti

Mvutano wa madaraka

Abdi Ayante, mkurugenzi wa taasisi ya turathi kwa ajili ya mitaala ya utafiti wa sera katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu, amesema kifo cha Godane kitaleta mabadiliko ya utaratibu kwa njia nyingi kwa kundi la al-Shabaab.

"Kile ambacho huenda kikatokea ni mvutano wa kuwania madaraka," amesema siku moja kabla ya wizara ya ulinzi ya Marekani kuthibitisha kifo cha Godane. Ayante amesema kuvunjika vipande kwa kundi hilo pia kunawezekana kutokana na kutokuwapo kwa kiongozi mwenye ujuzi kama Godane na mwenye kuchukua msimamo mkali dhidi ya upinzani.

"Alikuwa kiongozi imara wa al-Shabaab ... na kimsingi amewashughulikia mahasimu wake kikamilifu," amesema Matthew Olsen, mkurugenzi wa kituo cha taifa cha kupambana na ugaidi nchini Marekani.

Al-Shabaab ni kundi , lenye "vikundi vingi ndani yake" na " kuna idadi kubwa ya viongozi watarajiwa" wenye uwezo wa kuchukua nafasi ya Godane, Olsen amewaambia waandishi habari.

rais wa Marekani Barack ObamaPicha: picture alliance/AP Photo

Majeshi ya Marekani yalishambulia eneo alipokuwapo Godane katika eneo la kusini kati nchini Somalia kwa makombora pamoja siku ya Jumatatu, lakini wizara ya ulinzi haikuweza kuthibitisha kifo chake hadi jana Ijumaa (05.09.2014) ikisema bado inatathmini matokeo ya shambulio hilo.

Somalia yatangaza msamaha kwa wapiganaji

Rais wa Marekani Barack Obama , akihudhuria mkutano wa NATO nchini Wales , amedokeza kwa waandishi habari juu ya kuthibikika kwa kifo cha Godane, akisema : "tumetangaza leo ukweli kwamba tumemuua kiongozi wa al-Shabaab nchini Somalia.

Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud amethibitisha kuuwawa kwa Godane, akisema majeshi ya Marekani yamefanya shambulio hilo la anga kwa makubaliano na serikali ya Somalia ilikuwa inafahamu kikamilifu juu ya shambulio hilo.

Katika taarifa , Mohamud amesema kuwa wakati watu wenye msimamo mkali zaidi wanaweza kugombania madaraka ya kundi la al-Shabaab , serikali yake iko tayari kutoa msamaha wa siku 45 kwa wapiganaji wa al-Shabaab ambao watataka kujitenga kutoka kundi hilo la lenye mahusiano na al-Qaeda.

Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud (kulia) na catherine Ashton(shoto)Picha: picture-alliance/dpa

"Wale watakaoamua kubaki wanajua hatima yao. Al Shabaab inaporomoka," amesema rais huyo wa Somalia, na kuongeza: "Nawaambia wanachama wa al Shabaab : Godane amekufa na sasa ni nafasi kwa wanachama wa al Shabaab kukumbatia amani."

Serikali ya Somalia, ikipata msaada kutoka wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika na taarifa za kijasusi za mataifa ya magharibi, imekuwa ikipambana kudhibiti ushawishi wa al-Shabaab na kuliondoa kundi hilo kutoka maeneo ambayo imeendelea kuyathibiti tangu kuondolewa kutoka mji mkuu wa Mogadishu mwaka 2011.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre

Mhariri : Sudi Mnette