1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yatishia mashambulizi zaidi Syria

8 Aprili 2017

Marekani imeonya siku ya Ijumaa kuwa iko tayari kuishambulia tena Syria, baada ya shambulizi la makombora lililoikarisha Urusi na kuchochea miito ya kumalizwa kwa vita vilivyodumu kwa miaka sita nchini humo.

U.S. NavyZerstörer USS Ross (DDG 71) fires a tomahawk land attack missile in Mediterranean Sea
Picha: Reuters/Robert S. Price/Courtesy U.S. Navy

Balozi wa Marekani Nikki Haley alitoa onyo hilo wakati wa kikao cha dharura cha baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, kilichotishwa baada ya mashambulizi hayo, yaliofanywa kuadhibu kilichodaiwa kuwa shambulizi la kemikali lililofaywa na utawala wa Bashar al-Assad.

"Marekani ilichukuwa hatua iliozingatiwa vizuri usiku uliopita. Tuko tayari kufanya zaidi lakini tunatumai hilo halitohitajika. Ni wakati kwa mataifa yote yaliostaarabika kukomesha ukatili unaoendelea nchini Syria na kudai suluhisho la kisiasa," alisema Haley katika kikao cha dharura cha baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.

Mshirika wa Assad, Urusi wakati huo iliyatangaza mashambulizi ya kwanza ya Rais Donald Trump dhidi ya utawala wa Damascus, kuwa ukiukaji wa sheria ya kimataifa na kitendo cha uvamizi. Haley amesema mashambulio hayo yaliharibu kiwanja cha ndege ambako Washington inaamini serikali ya Syria ilianzishia shambulizi dhidi ya mji unaoshikiliwa na waasi wa Khan Sheikhun, ambako watu 86 walikufa wiki hii, wakiwemo watoto 27.

Mabaki ya ndege ya kivita ya Syria ilioharibiwa katika mashambulio ya makombora ya Marekani 07.04.2017.Picha: picture-alliance/dpa/Sputnik/M. Voskresenskiy

Urusi kuimarisha ulinzi wa angani Syria

Ofisi ya Assad iliataja mashambulizi ya Marekani kuwa ya "kipumbavu na yasio ya uwajibikaji", na Moscow ilitangaza hatua kadhaa za kujibu ikiwemo kuimarisha ulinzi wa anga la Syria. Haley alisema Marekani haitamsubiri tena Assad kutumia silaha za kemikali bila kuwepo na madhara, na kuonya kuwa siku hizo zimekwisha.

Marekani haikuomba ridhaa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya hatua hiyo ya kijeshi iliyofuatia siku kadhaa za hasira duniani kote baada ya kutolewa picha za watoto waliofariki kutokana na shambulio hilo linaloshukiwa la gesi aina ya sarin.

Huo ndiyo ulikuwa uamuzi mkubwa zaidi wa kijeshi wa Trump tangu alipoingia madarakani na uliashiria kuongezeka kwa ghafla kwa ushiriki wa Marekani katika vita vya muda mrefu nchini Syria.

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson, ambaye anatarajiwa kuizuru Moscow wiki ijayo kwa ajili ya mazungumzo na rais Vladmir Putin, alisema amesikitishwa na majibu ya Urusi kwa mashambulizi ya Marekani, kwa sababu yameonyesha kuendelea kwao kuunga mkono utawala wa Assad.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Harley akionesha picha za watoto waliokufa kutokana na shambulio la sumu nchini Syria.Picha: Reuters/S. Stapelton

Je, Urusi ilishiriki katika shambulio la kemikali?

Mjini Washington, afisa wa ngazi ya juu alisema huenda Syria ilipata usaidizi katika kutekeleza shambulizi hilo, lakini alisita kuitaja Urusi kuwa mshirika katika unyama huo. Wakati akitishia mashambulizi zaidi, Haley alisema ni wakati wa kuendelea na juhudi za kidiplomasia ili kufanikisha suluhisho la kisiasa kukomesha vita hivyo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitaka kuwepo na kujizuwia na msukumo mpya kwa amani nchini Syria, akisema hakuna njia ya nyingine ya kutatua mgogoro huo kuliko suluhu ya kisiasa.

Uingereza, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Israel, Japan, Saudi Arabia na Uturuki zote ziliunga mkono hatua ya Marekani, huku Ankara ikitaka kuundwe eneo lisiloruhusiwa kuruka ndege.

Mwandishi: Iddi Ssessanga

Mhariri: Daniel Gakuba

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW