Marekani yatoa msamaha wa muda kwa mafuta ya Urusi
13 Machi 2026
Uamuzi huo uliotangazwa na waziri wa fedha Scott Bessent, unalenga kutuliza masoko ya nishati duniani ambayo yamevurugika pakubwa kutokana na vita vinavyoendelea kati ya Iran na washirika Marekani na Israel.
Msamaha huo unahusu mafuta yaliyopakiwa kwenye meli tarehe 12 mwezi Machi au kabla yake na utadumu hadi Aprili 11 saa sita usiku kwa saa za Marekani. Uamuzi wa kutoa msamaha umefanyika katika wakati ambapo masoko ya mafuta yametikiswa na mgogoro unaendelea Mashariki ya Kati.
Mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran yamesababisha kuvurugika kwa usafirishaji wa mafuta kupitia Mlango Bahari wa Hormuz, njia muhimu kwa karibu theluthi moja ya mafuta yanayosafirishwa duniani. Hali hiyo imesababisha bei za mafuta ghafi kupanda hadi zaidi ya dola 100 kwa pipa, japo bei zilianza kushuka kidogo masoko ya Asia baada la tangazo la Washington.
Mapipa milioni 100 yanaweza kuathirika
Shirika la Kimataifa la Nishati IEA limesema msukosuko unaoshuhudiwa sasa ndio usumbufu mkubwa zaidi wa usambazaji wa mafuta kuwahi kutokea katika historia.
Kulingana na mjumbe maalum wa rais wa Urusi kuhusu ushirikiano wa kiuchumi, Kirill Dmitriev, msamaha huo unaweza kuathiri takriban mapipa milioni 100 ya mafuta ghafi ya Urusi yaliyoko baharini, kiasi ambacho ni karibu na matumizi ya dunia kwa siku moja.
Moscow imekaribisha uamuzi huo wa Washington, ikisema inaonyesha kuwa mafuta ya Urusi bado ni muhimu kwa utulivu wa masoko ya nishati duniani.
Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amesema, "Tunaona hatua ya Marekani kama jitihada za kuleta utulivu katika masoko ya nishati, na katika hilo, maslahi yetu yanafanana. Tumepokea maelezo kutoka kwa wawakilishi wa Marekani kwamba msamaha huu unahusu tu mafuta yaliyopakiwa kwenye meli kabla ya Machi 12. Hata hivyo, tumearifiwa kuwa, kwa ujumla, Marekani haina mpango wa kuondoa vikwazo vingine vyovyote vya mafuta dhidi ya Shirikisho la Urusi."
Waziri wa Fedha wa Marekani ameweka wazi kwamba uamuzi huo ulifikiwa kwa uangalifu mkubwa na ni wa muda tu, akisisitiza kwamba hautaleta faida kubwa ya kifedha kwa serikali ya Urusi.
Ameongeza kuwa uamuzi huo ni sehemu ya juhudi pana za kulinda watumiaji na biashara za Marekani dhidi ya kupanda kwa kwa gharama za nishati, hasa wakati shinikizo la kisiasa linaongezeka kuelekea uchaguzi wa katikati ya muhula mwezi Novemba, ambapo Warepublican wanatarajia kudumisha udhibiti wa Bunge.
Msamaha huo ni hatua ya pili kubwa ya kulegeza vikwazo vinavyohusiana na Urusi ndani ya muda mfupi na umeibua maswali chungunzima kuhusu uimara wa kampeni ya mataifa ya Magharibi ya kupunguza mapato ya nishati ya Moscow.
Ulaya yajibu kwa wasiwasi mkubwa
Mapato ya nishati ya Urusi yanaripotiwa kupungua sana katika miezi miwili ya kwanza ya mwaka, na hivyo kupanda kwa bei za mafuta kunaweza kuleta nafuu kwa Kremlin.
Hata hivyo viongozi wa Ulaya wameonyesha kutoridishwa na uamuzi huo wa Marekani. Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz amesema kulegeza vikwazo dhidi ya Urusi "sio hatua sahihi" akionya kwamba Moscow haipaswi kuruhusiwa kutumia mgogoro wa Iran kuimarisha vita vyake nchini Ukraine.
"Tulijadili pia suala la usambazaji wa mafuta na gesi kutoka Urusi na Rais wa Marekani wiki hii wakati wa mkutano wa wakuu wa nchi wa G7. Wanachama sita wa G7 walikuwa wazi kabisa kwamba hatua hiyo inatuma ishara mbaya. Tumejulishwa leo asubuhi kwamba serikali ya Marekani imeamua kutoa msamaha. Kwa mara nyingine tena: tunaamini kuwa hii sio hatua sahihi."
Waziri wa Uchumi wa Ujerumani Katherina Reiche pia ameonyesha wasiwasi kwamba hatua hiyo inaweza kuongeza fedha katika hazina ya vita ya Rais Vladimir Putin.
Kansela huyo wa Ujerumani ameeleza suala hilo lilijadiliwa wakati wa mazungumzo ya hivi karibuni ya viongozi wa G7 na Rais Donald Trump, na akabainisha kuwa wanachama sita kati ya saba walipinga uamuzi huo wa kulegeza vikwazo.
Waziri Mkuu wa Norway Jonas Gahr Store pia ameukosoa uamuzi wa Marekani, akisema Oslo ina mashaka makubwa kuhusu hatua yoyote ya kulegeza vikwazo vya mafuta dhidi ya Urusi wakati vita nchini Ukraine vinaendelea.