Marekani yatoa tahadhari kwa raia wake kuelekea Rwanda
8 Oktoba 2024Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani imesema viwango vya tahadhari hiyo vimepanda na kufikia hatua ya tatu, ikimaanisha raia wake ni lazima wafikirie kabla ya kukata shauri la kuelekea Rwanda. Kiwango kikifikia cha nne, huwa ni onyo kwa raia wa nchi iliyotoa tahadhari hiyo, kutosafiri kabisa katika nchi iliyohatari kiafya au kiusalama. Kulingana na wizara ya afya ya Rwanda watu 41 wameaambukizwa virusi hivyo, huku vifo vya watu 12 vikiripotiwa wengi wao wakiwa wahudumu wa afya, tangu kulipotokea mripuko wa Marburg nchini humo tarehe 27 Septemba.
Rwanda: Watu 11 wafa kwa Marburg
Huku hayo yakiarifiwa waziri wa wizara hiyo Nsanzimana Sabin amesema Rwanda itaanza kutoa chanjo siku ya Jumapili dhidi ya virusi hivyo vya Marburg vinavyofanana na Ugonjwa wa Ebola. Ameongeza kuwa tayari wamepokea dozi 700 za chanjo hiyo kutoka Marekani.
"Tumepokea chanjo, jana usiku dozi 700 ziliwasili kutoka taasisi ya chanjo ya Sabin. Chanjo itaanza kutolewa mara moja tumeangalia ubora wake na chanjo yenyewe iko sawa. Tutaanza kwa kuwapa kipaumbele wale walio katika hatari zaidi ya kuambukizwa, tuna wahudumu wa afya wanaofanya kazi katika vituo vya afya, hospitalini na hata katika vyumba vya wagonjwa mahututi na hata wale wanaokaribiana na wagonjwa," alisema waziri Nsanzimana.
Rwanda imeweka mikakati ya kudhibiti virusi vya Marburg
Chanjo hiyo ambayo majaribio yake yako katika awamu ya pili ilitolewa na taasisi ya chanjo iliyoko Marekani. Tasisi hiyo imesema majaribio pia ya chanjo hiyo inaendelea katika nchi jirani ya Uganda na Kenya na hakuna hatari yoyote iliyoripotiwa hadi sasa. Virusi hivyo hatari vinavyosababisha homa kali, kuharisha damu na kutapika vinasemekana pia kusababisha kufeli kwa viungo vya ndani vya mwili.
Watu 6 wafariki kwa virusi vya Marburg nchini Rwanda
Katika kudhibiti virusi hivyo Rwanda imeweka mikakati ya kupambana navyo ikiwemo marufuku ya kukusanyika kwa makundi na maziko ya watu wengi. Bodi ya maendeleo ya Rwanda imesema kuanzia siku ya Jumapili itaanza kuweka mikakati ya safari katika kukabiliana na virusi vya Marburg. Bodi hiyo pia imesema vipimo vya homa, kujaza fomu za afya, na vitakasa mikono vitaanza kutumika katika maeneo ya kusafiri na kutoa wito kwa wasafiri kufuatilia hali zao na kujua kama wana homa au la.
Marburg inaaminika kutoka kwa popo na kuingia kwa wanadamu na ni miongoni mwa virusi vinavyotoka kwa familia ya Filo inayojumuisha pia virusi vya Ebola.
afp/ap