1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaunda kundi la kuibana Iran

Yusra Buwayhid
17 Agosti 2018

Waziri wa Kigeni wa Marekani Mike Pompeo, Alhamisi, ametangaza kuundwa jopo maalumu la kusimamia mkakati wa Marekani dhidi ya Iran, wa kuilazimisha Jamhuri hiyo ya Kiislam kufanya mabadiliko makubwa katika uongozi wake.

USA Aktionsgruppe für Iran Mike Pompeo und Brian Hook
Picha: picture-alliance/AP Images/C. Owen

Akiishutumu Iran kwa kuanzisha vurugu dhidi ya Marekani, washirika wake, pamoja na raia wa wake wenyewe, Pompeo ametangaza kuundwa kwa jopo hilo ambalo amesema litasimamia utekelezaji wa sera za Marekani dhidi ya Iran mjini Washington pamoja na nje ya nchi.

"Matarajio yetu ni kwamba siku moja tutaweza kufikia makubaliano na Iran lakini kwanza tunataka kuona mabadiliko makubwa yakifanyika ndani ya serikali yake, pamoja na nje ya mipaka yake," amesema Pompeo akizungumza katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani. "Raia wa Iran na dunia kwa jumla wanataka kuiona Iran ikiendeshwa kama taifa lengine la kawaida."

Jopo hilo litaongozwa na Brian Hook, ambaye kwa sasa ni mkurugenzi wa mipango na sera katika wizara ya mambo ya nje ya Marekani.

Tokea ilipojitoa kutoka katika makubaliano ya kinyuklia, uongozi wa Trump umeiwekea tena vikwazo Iran ambavyo viliondoshwa chini ya makubaliano hayo.

Iran na nchi nyinginezo zilizoweka saini makubaliano hayo ya 2015,  ikiwa ni pamoja na Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Urusi na China wamekuwa wakitafuta njia ya kuyanusuru makubaliano yao, hata baada ya Marekani kuanza kuiwekea tena vikwazo Iran.

Khamenei akana uwezekano wa mazungumzo na Iran

Kiongozi wa kidini Iran, Ali KhameneiPicha: Reuters/Official Khamenei website

Hook amesema Pompeo ameainisha mambo 12 tofauti ambayo Iran inatakiwa kuyabadilisha katika uongozi wake, na ikifanya hivyo Trump atakuwa tayari kufanya mazungumzo nayo.

"Tumechukua hatua hii dhidi ya Iran kwa sababu upeo wa shughuli zake za uharibifu ni mpana sana. Kutoka silaha za nyuklia, msaada wake kwa ugaidi, shughuli zake za mtandaoni, kujiimarisha kwake kwa makombora na mengine mengi, utawala wa Iran umekuwa ukishochea vurugu na kuhatarisha utulivu. Mkakati wetu mpya utakabiliana na vitisho vyote vya Iran, na jopo hilo la Iran Action litakuwa na jukumu la kutekeleza mkakati huo," amesema Hook akizungumza katika Wizara ya Mambo ya Nje mjini Washingto, Marekani.

Kiongozi mkuu wa kidini nchini Iran Ayatollah Ali Khamenei, Ijumatatu iliyopita amekana uwezekano wowote ule wa kufanyika mazungumzo kati ya nchi yake na Marekani.

Baada ya Marekani kuiwekea vikwazo Iran hivi karibuni, serikali ya Trump imewatahadharisha wafanyabiashara pamoja na serikali za nchi za Umoja wa Ulaya kwamba itawaadhibu iwapo wataendelea kufanya biashara na Iran.

Hook amesema inazitaka nchi zote ziungane na Marekani katika suala hilo na ziachane na kununua mafuta ya Iran.

Marekani inapanga kuilazimisha Iran kusitisha mpango wake wa kutengeneza silaha za nyuklia na kuyaunga mkono makundi ya wanamgambo katika Mashariki ya Kati, ambako Iran imejitumbukiza katika vita vinavyoendelea nchini Yemen na Syria.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/dpa/ap/rtre

Mhariri:Iddi Ssessanga