1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yawadondoshea silaha Wakurdi

20 Oktoba 2014

Jeshi la Marekani limedondosha silaha, masanduku ya risasi na vifaa vya matibabu kwa Wakurdi wanaopigana na wanamgambo wa Dola la Kiislamu - IS mjini Kobane katika mpaka wa Syria

Kobane Gefechte IS 19.10.2014
Picha: Bulent Kilic/AFP/Getty Images

Hiyo ni mara ya kwanza kwa Marekani kudondosha kutoka angani silaha za kuwaisaidia wapiganaji wa Kikurdi wanaojaribu kuulinda mji wa Kobane dhidi ya kuangukia mikononi mwa wanamgambo wenye itikadi kali za kiislamu – IS. Hatua hiyo inaashiria kuongezeka juhudi za Marekani kuyaunga mkono majeshi ya upinzani ya Syria dhidi ya wanajihadi pamoja na utawala wa Rais wa Syria Bashar al-Assad

Wapiganaji wa Kikurdi wamekuwa wakishambuliwa na IS kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa mjini Kobane, ambao unapiganiwa wakati waandishi wa habari wa kimataifa wakishuhudia katika upande wa pili wa mpaka nchini Uturuki.

Afisa mkuu wa utawala wa Marekani amesema Wakurdi walihitaji msaada “mahsusi” na wa “dharura”. Ndege ya mizigho aina ya C-130 ilidondosha vifaa hivyo bila upinzani wowote kutoka ardhini. Afisa huyo amesema ndege hiyo ya mizigo haikuandamana na ndege zozote za kivita na baada ya operesheni hiyo iliondoka katika eneo hilo kwa usalama.

Wapiganaji wa Kikurdi wanaojaribu kuulinda mji wa Kobane dhidi ya wanamgambo wa ISPicha: AFP/Getty Images/Aris Messinis

Msaada huo umetolewa wakati wapiganaji wa IS wakiripotiwa kupata hasara kubwa hapo jana kutokana na mashambulizi ya mfululizo ya kutokea angani yanayofanywa na jeshi la muungano likiongozwa na Marekani.

Imeripotiwa kuwa “mamia” ya wapiganaji wa Dola la Kiislamu wameuawa katika mashambulizi hayo ya Kobane na “vifaa kadhaa pamoja na ngome za wapiganaji hao” kuharibiwa kabisa. Marekani na washirika wake wa magharibi wamekuwa wakiishinikiza Uturuki kuchukua jukumu la moja kwa moja la kupambana na IS mjini Kobane. Lakini Uturuki inasita kuingilia kati kijeshi au kuwapa silaha Wakurdi, ambao wamekuwa maadui wa kihistoria wakidai taifa huru ikiwa ni pamoja na maneo ya kusini mashariki mwa Uturuki.

Rais wa Uturiki Recep Tayyip Erdogan hapo jana tena amekataa wito wa kuitaka nchi yake kutoa silaha kwa Chama kikuu cha Kikurdi nchini Syria, akilitaja kundi hilo kuwa la kigaidi.

Alipoulizwa kama serikali ya Uturuki ilifahamishwa mapema kabla ya kudondosha vifaa vya msaada, afisa wa ngazi ya juu katika serikali ya Marekani alisema Rais Barack Obama alizungumza na Erdogan siku ya Jumamosi, “na aliweza kumfahamisha kuhusu nia yao ya kufanya hivyo pamoja na umuhimu wake”.

Afisa huyo aliongeza kuwa Marekani inafahamu kuhusu wasiwasi ambao Uturuki imekuwa nao kwa muda mrefu na makundi kadhaa yakiwemo ya Kikurdi, lakini kundi la Dola la Kiislamu ni “adui wa pamoja” kwa Marekani na Uturuki.

Mwandishi: Bruce Amani
Mhariri: Josephat Charo