1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yawawekea vikwazo maafisa wa Rwanda na Kongo

Saleh Mwanamilongo
25 Agosti 2023

Miongoni mwa waliowekewa vikwazo ni pamoja na maafisa wawili wa jeshi la Rwanda na Kongo pamoja na viongozi wanne wa makundi ya waasi ya M23 na FDLR.

Marekani yawawekea vikwazo watu 6 wakiwemo viongozi wa waasi wa FDLR kwa dhima yao katika vita vya Kongo
Marekani yawawekea vikwazo watu 6 wakiwemo viongozi wa waasi wa FDLR kwa dhima yao katika vita vya KongoPicha: DW/S. Schlindwein

Taarifa ya wizara ya fedha ya Marekani imesema waliowekewa vikwazo ni pamoja na jenerali Andrew Nyamvumba kutoka jeshi la Rwanda la RDF, kanali wa jeshi la Kongo Salomon Tokolonga, Bernard Byamungu makamu kamanda wa waasi wa M23, na watatu wengine Apollinaire Hakizimana, Sebastian Uwimbabazi na Protogene Ruvugayimikore ambao ni viongozi wa waasi wa FDLR.

Jenerali Nyamvumba moja ya makamanda wa jeshi la Rwanda ametuhumiwa kuwaunga mkono waasi wa Kongo wa M23. Huku kanali Salomon Tokolonga wa jeshi la Kongo akituhumiwa kushirikiana na makundi ya waasi likiwemo lile la FDLR katika kupambana na uasi wa M23 huko Kivu ya Kaskazini.

Kuzuwiliwa kwa mali za wahusika

Brian Nelson, afisa anayehusika na kupambana na ufadhili wa ugaidi kwenye wizara ya fedha ya Marekani alisema vikwazo hivyo vinaonyesha kujitolea kwa Marekani kuendeleza juhudi za kutatua mgogoro na kushughulikia hali mbaya ya kibinadamu huko mashariki mwa Kongo.

Nelson aliendelea kusema kuwa pande zote kwenye mzozo, huko mashariki mwa Kongo, zinahusika na ukiukwaji wa haki za binadamu ikijumisha unyanyasaji wa kijinsia.

Miongoni mwa vikwazo ni pamoja na kuzuwiliwa kwa mali na maslahi yote ya wahusika hao nchini Marekani pamoja na kutoruhusiwa kuingia nchini humo.

Marekani yazitaka Rwanda, Kongo kuutuliza mvutano 

Blinken kamshinikiza Kagame kutulizaa uhasama baada ya kuzuka mivutano mipya kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya KongoPicha: Andrew Harnik/AFP/Getty Images

Vikwazo hivyo dhidi ya maafisa wa jeshi la Rwanda, Kongo pamoja na viongozi wa waasi wa M23 na FDLR vimetolewa siku kadhaa baada ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken kufanya mazungumzo na Rais wa Rwanda Paul Kagame na kushinikiza kutulizwa kwa uhasama baina ya Rwanda na Kongo.

Pia wiki hii, ujumbe wa wabunge wa kamati ya mambo ya nje ya bunge la Marekani wamezuru Kongo na kuhimiza kurejea kwa amani na maandalizi bora ya uchaguzi mkuu wa Desemba.

Kongo yakanusha ukandamizaji wa upinzani

Wakati huohuo serikali ya Kongo ilikanusha shutuma za shirika la Human Rights Watch kwamba upinzani unakabiliwa na vitisho na ukandamizaji katika maandalizi ya uchaguzi wa rais.

Wizara ya Kongo ya mawasiliano ilitupilia mbali madai hayo na kushutumu kile ilisema ni baadhi ya wapinazani ambao wanajaribu kuvuruga maandalizi ya uchaguzi. Wiki hii, shirika la Human Rights Wacth lilituhumu kamatakamata dhidi upinzani huku ikisalia miezi minne kabla ya uchaguzi wa rais, bunge na madiwani.