1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yawawekea vikwazo maafisa wa China na Hong Kong

17 Machi 2021

Marekani imeweka vikwazo kwa maafisa zaidi 24 wa China na Hong Kong kutokana na ukandamizaji unaondelea kufanywa na China dhidi ya uhuru wa kisiasa mjini Hong Kong.

USA Außenminister Antony Blinken
Picha: Andrew Caballero-Reynolds/REUTERS

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Anthony Blinken amesema hatua hiyo inatokana na wasiwasi mkubwa iliyonao Marekani kuhusu ukandamizaji wa demokrasia ya Hong Kong kutokana na mabadiliko katika sheria yake ya uchaguzi iliyoidhinishwa na bunge la China wiki iliyopita. Vikwazo hivyo vimewekwa kabla ya serikali ya Rais Joe Biden kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na China.

Marekani imeonya kuwa benki zake za kigeni sasa zimepigwa marufuku kufanya biashara yoyote ile na maafisa wa ngazi ya juu waliowekewa vikwazo hivyo. Tamko hilo limetolewa wakati wa ziara ya Blinken na Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Lloyd Austin nchini Japan na Korea Kusini.

Kamati kuteua wabunge

Mabadiliko hayo katika mfumo wa uchaguzi wa Hong Kong yanaipa kamati maalum inayoegemea upande wa serikali ya China mamlaka ya kuteua wabunge zaidi wa Hong Kong pamoja na kupunguza jukumu la umma katika serikali. Wote waliowekewa vikwazo hivyo ni maafisa wa juu wa chama cha Kikomunisti cha China pamoja na maafisa wakuu wa usalama wa taifa mjini Hong Kong.

Hata hivyo, China imekanusha madai ya kukiuka haki za binaadamu ikisema kuwa taarifa ya pamoja ya Marekani na Japan ni ''shambulizi la makusudi'' dhidi ya sera yake ya kigeni na inaingilia masuala ya ndani ya China. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa China, Zhao Lijian amesema China haijaridhishwa na taarifa hiyo na inaipinga vikali.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa China, Zhao LijianPicha: picture-alliance/Kyodo

''Vikwazo vya Marekani dhidi ya maafisa wa China kwa kuzingatia kile kinachoitwa ''Sheria ya Uhuru wa Hong Kong'' ni ukiukaji mkubwa wa sheria ya kimataifa na kanuni za msingi za uhusiano wa kimataifa na vinaingilia masuala ya ndani ya China na tutachukua hatua za lazima,'' alifafanua Lijian.

Soma zaidi: Je China itaondolewa vikwazo vya silaha na Umoja wa Ulaya?

Wakati huo huo, Umoja wa Ulaya umekubaliana kuwawekea vikwazo maafisa wanne wa China na kampuni moja ya nchi hiyo kutokana na ukandamizaji unaofanywa na China dhidi ya jamii ya watu wachache ya Uighur.

Wanadiplomasia wamesema kuwa hatua hiyo ambayo itathibitishwa na mawaziri wa mambo ya nje wa umoja huo kwenye mkutano wao wa Jumatatu, ni sehemu ya mpango wa kuweka vikwazo kutokana na ukiukaji wa haki za binaadamu, ambao utawalenga pia watu binafsi nchini Urusi, Korea Kaskazini, Eritrea, Sudan Kusini na Libya.

Vikwazo hivyo ni vipya dhidi ya China tangu vikwazo vya silaha vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya mwaka 1989, baada ya ukandamizaji katika Uwanja wa Tiananmen. Balozi wa China kwenye Umoja wa Ulaya, Zhang Ming amesema vikwazo hivyo vinatokana na uongo na huenda vikatafsiriwa kuwa vinahujumu makusudi maslahi ya usalama na maendeleo ya China.

(DPA, AP, AFP, Reuters)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW