Marekani yawawekea vikwazo viongozi wawili Zimbabwe
12 Machi 2020Marekani imewawekea vikwazo viongozi wawili wa Zimbabwe kwa ukiukaji wa haki za binadamu.Wizara ya fedha ya Marekani inaelezea kwamba viongozi hao walihusika na mashambulizi dhidi ya waandamanaji nchini humo.Hatua hiyo imekuja wiki moja tu baada ya Marekani kuongeza vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Zimbabwe kwa kipindi cha mwaka mmoja zaidi.
Taarifa ya wizara ya fedha ya Marekani imeeleza kuwa Waziri wa Usalama wa Zimbabwe, Owen Ncube amewekwa katika orodha ya watu waliowekewa vikwazo na Marekani kufutia tuhuma kwamba aliwaamuru maafisa wa usalama wa nchi hiyo kuwavamia na kuwatesa wanachama wa upinzani.
Kwa mujibu wa wizara hiyo, pia imemuwekea vikwazo Anselem Sanyatwe, Balozi wa Zimbabwe nchini Tanzania, ikimtuhumu kuongoza mashambulizi ya maafisa wa usalama dhidi ya wapinzani baada ya uchaguzi wa mwaka 2018. Wakati huo Sanyantwe alikuwa akiongoza kitengo cha ulinzi wa rais kwenye jeshi la taifa.
Kwenye taarifa yake waziri wa mambo ya nje wa marekani, Mike Pompeo aliitaka serikali ya Zimbabwe ''kukomesha haraka matumizi ya nguvu dhidi ya waandamanaji kwa njia ya amani, asasi za kiraia, viongozi wa vyama vya wafanyakazi na wanachama wa upinzani nchini humo, na kuendesha uchunguzi na kuwafikisha mbele ya vyombo vya kisheria wale wanaokiuka haki za binadamu''.
Vikwazo vya marekani havina msingi
Wandamanaji pamoja na watazamaji sita waliuliwa na wengine kadhaa walijeruhiwa mwaka 2018 baada ya kuahirishwa kutangazwa matokeo ya uchaguzi, ambayo yalimpa ushindi Emmerson Mnangagwa kama rais wa kwanza kuchaguliwa toka aondolewe madarakani Robert Mugabe.
Naibu waziri wa fedha wa Marekani, Justin Muzinich amesema viongozi wa kisiasa na wa kijeshi nchini Zimbabwe walitumia nguvu mara nyingi kuwanyamazisha wakosoaji na maandamano ya amani.
Vikwazo hivyo ni pamoja na kuzuwiya mali za viongozi hao wawili zilizoko nchini Marekani na vilevile kuzuwiya Wamarekani kutofanya nao shughuli zozote za kibiashara.
Mwaka 2019, Ncube na Sanyatwe waliwekewa vikwazo vya kutoizuru Marekani. Wiki iliyopita Marekani ilongeza vikwazo dhidi ya Zimbabwe kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa kile ilichoeleza kuwa ni mauwaji na ubakaji unaofanywa na maafisa wa usalama. Hatua hiyo ilipokelewa kwa huzuni na serikali ya Zimbabwe ambayo ilielezea kwamba tuhuma za Marekani hazina msingi.
Kwa takriban miaka ishirini sasa Marekani imeiwekea vikwazo Zimbabwe wakiwemo maafisa wake wa kisiasa na kijeshi. Rais wa sasa Emmerson Mnangagwa ni miongoni mwa viongozi waliowekewa vikwazo hivyo kwa tuhuma za kuwabana wapinzani.
Uhusiano baina ya Zimbabwe na Marekani umekuwa wa pandashuka toka utawala wa Robert Mugabe. Mwaka uliopita Zimbabwe ilimtuhumu balozi wa Marekani nchini humo kuwa na tabia kama ''mwanachama wa upinzani''.