1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yawekea vikwazo jeshi la Rwanda

3 Machi 2026

Marekani imeliwekea vikwazo Jeshi la Ulinzi la Rwanda na maafisa wake wanne waandamizi kwa tuhuma za kuunga mkono kundi la M23, ambalo linahusishwa na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu mashariki mwa DRC.

USA Washington D.C. 2025 | Trump bei Unterzeichnung des Friedensabkommens mit Ruanda und der DR Kongo
Picha: Andrew Caballero-Reynolds/AFP

Hatua hii imechukuliwa licha ya makubaliano ya amani yaliyosainiwa mwezi Desemba mjini Washington kati ya Rais Félix Tshisekedi wa Congo na Rais Paul Kagame wa Rwanda, chini ya usimamizi wa Rais wa Marekani Donald Trump.

Wakati huo, Trump aliwasifu viongozi hao kwa ujasiri wao, huku makubaliano hayo pia yakifungua hifadhi muhimu za madini za eneo hilo kwa serikali na makampuni ya Marekani.

Licha ya makubaliano hayo, mapigano kati ya pande hizo mbili yanaendelea katika maeneo kadhaa mashariki mwa Kongo, yakisababisha vifo vya raia na wanajeshi wengi.

Ofisi ya Udhibiti wa Mali za Kigeni (OFAC) chini ya Wizara ya Fedha ya Marekani imesema mashambulizi ya M23 yasingewezekana bila msaada wa moja kwa moja kutoka kwa serikali ya Rwanda.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Thomas Pigott, amesema M23 "inahusika na ukiukwaji wa kutisha wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na mauaji ya papo kwa papo na ukatili dhidi ya raia, wanawake na watoto.”

Maafisa waliolengwa na vikwazo ni pamoja na Mkuu wa Majeshi ya RDF Vincent Nyakarundi, Meja Jenerali Ruki Karusisi, Mkuu wa Ulinzi Mubarakh Muganga, na Kamanda wa Operesheni Maalum Stanislas Gashugi. 

Wanachama wa kundi la waasi la M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wakikagua silaha zilizosalimiswa na wanamgambo wa Wazalendo huko Uvira, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Picha: Daniel Buuma/Getty Images

Rwanda imepinga vikwazo hivyo, kupitia msemaji wake Yolande Makolo,imesema vinapotosha ukweli wa mgogoro na kuilaumu Congo kwa kukiuka makubaliano hayo.

M23 tayari iko chini ya vikwazo vya Marekani tangu mwaka 2013.

Uwanja wa ndege walengwa 

Wakati hayo yakijiri, mashambulizi ya ndege zisizo na rubani yameripotiwa katika uwanja wa ndege wa Kisangani, mji muhimu ulioko mbali na mstari wa mbele wa mapigano.

Serikali ya jimbo la Tshopo imesema droni nne zilidunguliwa karibu na uwanja wa ndege huo siku ya Jumapili, wakati ndege ya abiria ikijiandaa kutua. Hata hivyo hakuna uharibifu wala majeruhi, ingawa mashahidi walisikia milipuko na milio ya risasi iliyosababisha taharuki kwa wafanyakazi na wakazi wa eneo hilo.

Kundi la AFC/M23, ambalo Umoja wa Mataifa unasema linaungwa mkono na Rwanda, limekuwa likipanua udhibiti wake mashariki mwa Congo baada ya mashambulizi ya kasi mwaka jana yaliyowapa udhibiti wa miji ya Goma na Bukavu. Madai ambayo Rwanda imeendelea kukanusha.

Mgogoro mashariki mwa Congo umeendelea kuwa miongoni mwa misukosuko mikubwa zaidi ya kibinadamu duniani, ukiwasukuma zaidi ya watu milioni saba kukimbia makazi yao. Licha ya juhudi za upatanishi zinazoongozwa na Qatar na Marekani, mapigano bado yanaendelea katika maeneo kadhaa ya mashariki mwa nchi.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW