1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yawekwa orodha ya demokrasia zinazorudi nyuma

22 Novemba 2021

Ripoti ya taasisi ya kimataifa ya IDEA imeiweka Marekani kwenye orodha ya mataifa yanayorejea nyuma kidemokrasia kwa mara ya kwanza, inayoashiria kuporomoka vibaya kwa taifa hilo kulikoanza mwaka 2019.

USA Wahlen Poster
Picha: Imago/IPON

Kilimwengu, mtu mmoja katika kila watu wanne anaishi katika taifa ambalo demokrasia yake inarudi nyuma, huku wawili katika kila watatu wakiishi kwenye tawala za kiimla ama mfano wake, inasema ripoti ya Taasisi hiyo ya Demokrasia na Usaidizi wa Uchaguzi yenye makao yake makuu Stockholm, Sweden. 

Kushirikishwa kwa Marekani miongoni mwa mataifa yanayofanya vibaya kidemokrasia ni jambo lililowashituwa wengi.  

Mmoja wa waandishi wa ripoti hiyo iliyopewa jina la "Hali ya Demokrasia Ulimwenguni 2021", Alexander Hudson, alisema hilo linatokana na kuporomoka kwa mifumo ya uangalizi na usimamizi serikalini ambayo inaashiria matatizo makubwa kwenye misingi ya demokrasia, hata kama kwenye kiwango cha juu, Marekani bado inafanya vizuri sana katika demokrasia, ikiwemo kuimarisha mifumo ya viashiria vya utawala usiopendelea mwaka 2020. 

"Mwaka huu, tumeiweka Marekani kwenye orodha ya mataifa yanayorudi nyuma kidemokrasia kwa mara ya kwanza, lakini takwimu zetu zinaonesha kuwa matukio ya kurejea nyuma yalianza mwaka 2019." Alisema Hudson.

Viongozi wa kiraia waliopinduliwa nchini Myanmar.Picha: AFP/Getty Images

Hudson aliliambia shirika la habari la AFP kwamba demokrasia ya Marekani ilipata kubwa zaidi baina ya mwaka 2020 na 2021, pale aliyekuwa rais wa taifa hilo, Donald Trump, alipohoji uhalali wa matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2020, ambao ulimuondoa madarakani. 

Jambo jengine lililodhihirisha kurudi nyuma kwa demokrasia ya Marekani, kwa mujibu wa ripoti hiyo ya IDEA, ni kiwango cha uhuru wa kujikusanya na maandamano katika majira ya kiangazi ya mwaka 2020, yaliyofuatia kifo cha George Floyd.

Mwaka wa tano mfululizo demokrasia yarudi nyuma

Taasisi ya kimataifa ya IDEA huelekeza uchambuzi wake kwenye miaka 50 ya viashiria vya demokrasia kwenye mataifa 160 kwa kutumia vigezo vitatu vya serikali za kidemokrasia, tawala za kiimla na tawala zinazofanana ama na demokrasia ama uimla.

Katibu mkuu wa taasisi hiyo, Kevin Casas-Zamora amesema kwamba ugunduzi wa hali ilivyo Marekani ni jambo la kushitusha, akionya kwamba athari ya uamuzi wa Trump kukataa matokeo ya uchaguzi bila kuwa na ushahidi ilisambaa hadi Myanmar, Peru na Israel. 

Maandamano ya umma nchini SudanPicha: Ashraf Idris/AP Photo/picture alliance

Idadi ya mataifa yaliyorejea nyuma kidemokrasia imeongezeka maradufu ndani ya kipindi cha muongo mmoja, ambapo sasa ni takribani robo ya dunia. Mbali na Marekani, mataifa mengine yaliyomo kwenye orodha hiyo ni wanachama wa Umoja wa Ulaya kama vile Hungary, Poland na Slovenia.

Mataifa mawili yaliyokuwamo kwenye orodha hiyo mwaka jana, Ukraine na Macedonia ya Kaskazini, zimeondolewa mwaka huu baada ya hali yao kuimarika. Mataifa mengine mawili, Mali na Serbia, yamendolewa kabisa kwenye orodha hiyo, kwani hayahisabiwi tena kuwa ya kidemokrasia.

Wakati Myanmar ikihama kabisa kutoka demokrasia kwenda kwenye uimla moja kwa moja, Afghanistan na Mali zimeingia kwenye orodha ya mfano wa serikali za kiimla.

Kwa ujumla, kwa mwaka wa tano mfululizo, orodha ya mataifa yanayoelekea kwenye udikteta imekuwa ikiipiku ya zile zinazoishi ama kuelekea kwenye demokrasia.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW