1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaYemen

Marekani yazindua muungano wa ulinzi wa Bahari ya Shamu

19 Desemba 2023

Waziri wa ulinzi Lloyd wa Marekani Austin, amesema nchi yake inaongoza operesheni ya kimataifa ili kulinda biashara katika Bahari ya Shamu dhidi ya mashambulizi ya waasi wa Houthi wa Yemen wanaoungwa mkono na Iran

Meli za kivita katika mlango-bahari wa Hormuz ndani ya Ghuba ya Uajemi siku ya Jumapili, Novemba 26, 2023, kama sehemu ya shughuli za kijeshi za Marekani katika Mashariki ya Kati wakati wa vita vya Israel na Hamas.
Meli za kivita katika mlango-bahari wa Hormuz ndani ya Ghuba ya Uajemi Picha: Ruskin Naval/U.S. Navy/AP Photo/picture alliance

Austin, ambaye yuko ziarani Bahrain, makao makuu ya jeshi la wanamaji la Marekani katika Mashariki ya Kati, amesema Uingereza, Bahrain, Canada, Ufaransa, Italia, Uholanzi, Norway, Ushelisheli na Uhispania, ni miongoni mwa mataifa yanayohusika katika operesheni hiyo ya usalama wa Bahari ya Shamu.

Soma pia:Wahouthi wazishambulia meli za Marekani kwa droni

Ufaransa ilisema baadaye kwamba itajiunga na juhudi hizo za kulikomesha kundi hilo la waasi.

Muungano unafanya doria za pamoja

Muungano huo, utafanya doria za pamoja katika eneo la Kusini mwa Bahari hiyo ya Shamu katika Ghuba ya Aden.

Katika taarifa, Austin amesema kwamba hii ni changamoto ya kimataifa inayohitaji hatua ya pamoja na kuutangaza muungano huo kama Msimamizi wa Operesheni ya Ufanisi.

Austin atoa wito kwa mataifa kuchangia katika juhudi za kulinda Bahari ya Shamu.

Soma pia:Waasi wa Yemen watishia kushambulia meli zinazoelekea Israel kutokea bahari ya shamu

Katika mkutano uliofanywa kwa njia ya video na mawaziri kutoka mataifa zaidi ya 40, Austin alitoa wito kwa nchi zingine kuchangia huku akilaani vitendo hivyo vya kundi hilo la Wahouthi.

Waasi wa HouthiPicha: Khaled Abdullah/REUTERS

Tangazo la Austin hata hivyo linaacha maswali mengi, ikiwa ni pamoja na mataifa mangapi yako tayari kufanya kile ambacho meli nyingi za kivita za Marekani zimefanya katika siku za hivi karibuni,  kudungua makombora na ndege zisozo na rubani za Wahouthina kutoa msaada kwa meli za kibiashara zinazoshambuliwa.

Baadhi ya makampuni yabadilisha njia ya safari zao

Kampuni za usafirishaji ziliendelea kugeuza njia ya safari zao baharini licha ya tangazo la Austin.

Kampuni ya Maersk ya Denmark, ambayo ilikuwa imesimamisha safari zake kupitia Bahari ya Shamu, imesema itapeleka meli zake kuzunguka kupitia Afrika hadi itakapotangaza tena.

Soma pia:Meli ya kivita ya Marekani yazuia mashambulizi ya Wahouthi

Meli nyingine nyingi bado zilikuwa zinapitia njia hiyo ya bahari. Meli kadhaa zinazotumia Bahari ya Shamu zimebeba walinzi wenye silaha.

Vyanzo vya sekta hiyo ya usafirishaji vinasema athari kwa biashara ya kimataifa itategemea muda ambao mgogoro huo utachukuwa lakini malipo ya  bima na njia ndefu zitakuwa changamoto za sasa hivi.

Waasi wa Houthi wasema hawatazuiwa na muungano huo mpya

Waasi wa Houthi, ambao wanadhibiti maeneo makubwa ya Yemen, wametishia kulenga meli zote zinazoelekea Israel, bila kujali utaifa wao, na kuonya makampuni ya kimataifa  dhidi ya kujishughulisha na bandari za Israeli. .

Kundi hilo limesema leo kuwa muungano huo unaoongozwa na Marekani hautawazuia.