1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaziondowa Ethiopia, Guinea na Mali kwenye AGOA

2 Januari 2022

Serikali ya Marekani imeanza rasmi kutekeleza agizo la Rais Joe Biden la kuziondowa Ethiopia, Mali na Guinea kutoka makubaliano ya kibiashara kati ya taifa hilo na Afrika kutokana na uvunjwaji wa haki za binaadamu.

USA Washington | Joe Biden
Picha: SHAWN THEW/Newscom/picture alliance

"Marekani hivi leo imeziondosha Ethiopia, Mali na Guinea kutoka kwenye programu ya biashara ya AGOA kutokana na vitendo vya kila serikali kwenye kuvunja Mkataba wa AGOA," ilisema Ofiis ya Mwakilishi wa Biashara wa Marekani kwenye taarifa yake iliyotolewa siku ya Jumamosi (Januari Mosi).

Mkataba uliopewa jina la Sheria ya Ukuwaji wa Uchumi na Fursa Barani Afrika (AGOA) ulianza kufanya kazi mwaka 2000 chini ya utawala wa rais wa wakati huo wa Marekani, Bill Clinton, kuwezesha na kusimamia biashara kati ya Marekani na Afrika.

Lakini taarifa hiyo inasema Marekani "inatiwa wasiwasi sana na mabadiliko ya serikali yanayokwenda kinyume na katika nchini Guinea na Mali na uvunjwaji mkubwa wa haki zinazotambuliwa kimataifa za binaadamu unaochochewa na serikali ya Ethiopia na pande nyengine wakati mzozo ukiongezeka kaskazini mwa Ethiopia."

"Kila nchi ina jukumu la wazi la kufuata njia ya kurejeshwa kwenye AGOA na serikali ya Marekani itashirikiana na serikali zao kufikia lengo hilo," ilisema taarifa hiyo ya Mwakilishi wa Biashara wa Marekani.

Athari kubwa kwa Ethiopia

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed (wa tatu kushoto) akiwa kwenye uwanja wa mapambano dhidi ya waasi wa kaskazini mwa nchi yake.Picha: Ethiopian Prime Minister's Office//AA/picture alliance

Hatua hiyo ya Marekani inatishia sekta ya viwanda vya nguo nchini Ethiopia, ambayo husambaza bidhaa kwa kampuni za nguo za fasheni duniani, na pia dhamira ya taifa hilo la Pembe ya Afrika kuwa kituo kikuu cha utengezaji bidhaa za viwandani.

Vile vile inaongeza mbinyo kwenye uchumi ambao tayari umeathirika kutokana na vita kaskazini mwa  nchi hiyo, janga la virusi vya corona na kupaa kwa bei ya bidhaa muhimu. 

Mnamo mwezi wa Novemba, Wizara ya Biashara ya Ethiopia ilisema imefadhaishwa sana na tangazo hilo la Washington, ikisema hatua hiyo "itayarejesha nyuma mafanikio ya kiuchumi yaliyokwishapatikana na kuwaathiri vibaya wanawake na watoto."

Chini ya makubaliano ya AGOA, maelfu ya bidhaa kutoka Afrika zinaweza kufaidika na punguzo la kodi kwa masharti kwamba serikali za mataifa husika zinaheshimu haki za binaadamu, utawala bora na ulinzi wa wafanyakazi pamoja na kutoweka marufuku ya ushuru kwa bidhaa za Marekani zinazoingia kwenye maeneo yao.

Kufikia mwaka 2020, mataifa 38 yalikuwa tayari kwenye mfumo huo wa AGOA, kwa mujibu wa tovuti ya Mwakilishi wa Biashara wa Marekani. 

Mkataba huo uliboreshwa mwaka 2015 na Baraza la Congress la Marekani, ambalo pia liliuongezea muda hadi mwaka 2025.