1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yazuia azimio la kusitisha mapigano Gaza

19 Septemba 2025

Marekani imetumia kura yake ya turufu Alhamisi kuzuia kupitishwa kwa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililotaka usitishwaji mapigano Gaza, kuwezesha ufikiaji wa misaada ya kiutu na kuachiliwa kwa mateka.

New York I Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York, MarekaniPicha: Loey Felipe/UN Photo/Xinhua/picture alliance

Azimio hilo ambalo rasimu yake ilianza kujadiliwa mwezi Agosti, iliungwa mkono na wanachama wote 14 wa baraza hilo ispokuwa Marekani ambayo ilipendekeza uwepo wa azimio la kibinaadamu pekee.

Lakini kwa mujibu wa duru za kidiplomasia, Ufaransa, Uingereza na Urusi zilitilia shaka faida na ufanisi wa azimio la kibinadamu pekee kutoka kwa chombo kilichoundwa kwa ajili ya kudumisha amani na usalama duniani.

Mwezi Juni, Marekani ilitumia pia kura yake ya turufu kuzuia azimio kama hilo ili kumlinda mshirika wake Israel. Mwanadiplomasia wa Marekani Morgan Ortagus ametetea uamuzi wa taifa lake akisema azimio hilo halikujumuisha kauli za kulaani vitendo vya Hamas na kuwa limeshindwa kutambua hali halisi na ukweli kwamba kumekuwa na ongezeko kubwa la mtiririko wa  misaada ya kibinadamu  katika Ukanda wa Gaza.

Mashambulizi ya Israel huko Gaza yaendelea kusababisha maafa makubwaPicha: Ebrahim Hajjaj/REUTERS

Hayo yanajiri wakati Israel imeendeleza operesheni yake kubwa ya kijeshi huko Gaza City huku maelfu ya Wapalestina wakiendelea kuondoka katika jiji hilo na kuelekea eneo la Kusini. Mamlaka za  Gaza  zimesema watu 85 wameuawa ndani ya muda wa saa 24 zilizopita.

Kundi la Hamas limesema limewasambaza mateka wa Israel katika wilaya kadhaa za mji wa Gaza na kwamba mashambulizi ya Israel katika mji huo yatahakikisha kuwa hakuna mateka yeyote atakayerejea Israel.

Ufaransa yakemea upanuzi wa makazi ya walowezi

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema kutambuliwa kwa taifa huru la Palestina ndiyo njia bora ya kuwatenga Hamas. Macron ameitoa kauli hiyo alipohojiwa mjini Paris na mwandishi wa habari wa  Israel  Yonit Levi huku akikemea pia vitendo vya Israel kutanua makazi ya walowezi:

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron Picha: Jacquelyn Martin/AP Photo/picture alliance

" Kuhusu upanuzi wa makazi ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi sio haki na ni kitendo cha kutowajibika. Si haki kwa sababu Ukingo wa Magharibi hauna uhusiano wowote na Hamas. Na watu wanapoanza kusema kuwa jibu lao kwa hatua ya kulitambua taifa la Palestina au kwa hali ilivyo litakuwa ni kuanzisha upya makazi katika Ukingo wa Magharibi, huu ni ushahidi tosha kwamba huu ni mpango wa kisiasa ambao lengo lake si kuitokomeza Hamas bali ni kuzuia uwezekano wa suluhisho la mataifa mawili na haki ya watu wa Palestina kuishi kwa amani katika eneo hilo."

Aidha Macron amesema hajawahi kuondoa uwezekano wa kufanya mazungumzo yenye tija ili kuutafutia suluhu mzozo huo na kwamba yuko tayari kuendelea kushirikiana na viongozi wa Israel ikiwa ni pamoja na rais Isaac Herzog na Waziri Mkuu  Benjamin Netanyahu.

// DPA, AP, Reuters, AFP

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW