1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Marekani,China na Urusi na Urusi kujadili ushirikiano leo

Angela Mdungu
7 Mei 2021

Wanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Marekani, China na Urusi, leo watashiriki mkutano wa baraza la usalama la Umoja wa mataifa unaoratibiwa na China inayoshikilia uenyekiti wa mzunguko wa baraza hilo kwa mwezi huu

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Antony Blinken na mwenziye wa Urusi Sergey Lavrov ni kati ya waliothibitisha kuwa watashiriki kwenye mkutano huo utakaofanyika kwa njia ya video ambapo waziri wa mambo ya nje wa China atakuwa mwenyekiti.

Akizungumzia mkutano huo msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya China Wang Wenbin amesema China inatumaini kuwa pande zote zikiwemo nchi wanachama wa baraza la usalama zitatumia mkutano huo kama nafasi ya kuonesha uthabiti wao katika ushirikiano wa kimataifa na uimara katika kusudi na misingi ya azimio la Umoja wa mataifa, kulinda mfumo wa kimataifa kwa kufuata sheria za kimataifa na kuendeleza amani na usalama wa kieneo.

Mapema Jumatatu mjumbe wa China katika Umoja wa Mataifa Zhang Jun, katika mkutano wake na wanahabari  alisema ni dhahiri kwamba ushirikiano wa kimataifa ni njia sahihi ya mapambano dhidi ya migogoro inayoikabili dunia.

Alirejelea azimio lililopitishwa mwezi Septemba mwaka uliopita wakati wa maadhimisho ya miaka 75 ya Umoja wa Mataifa linaloainisha kuwa kutokana na janga la COVID 19 ushirikiano wa mataifa siyo chaguo bali ni hitaji muhimu katika kujenga dunia yenye usawa zaidi, uvumilivu na endelevu zaidi.

Ushirikiano wa Marekani na nchi za Magharibi ni muhimu

Naye Rais wa Marekani Joe Biden, katika mkutano wa mwaka wa baraza la Usalama la umoja wa mataifa wa Munich uliofanyika mwezi Februari kwa njia ya video, aliorodhesha masuala yanayotia wasiwasi yakiwemo kufufua mazungumzo ya mpango wa nyuklia wa Iran na kukabiliana na changamoto kiuchumi na kiusalama zinazosababishwa na China na Urusi, pamoja na kushughulikia uharibifu uliotokana na janga la COVID 19 ambalo alisema linahitaji ushirikiano kati ya Marekani na washirika wake wa mataifa ya Magharibi.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Anthony BlinkenPicha: Valentyn Ogirenko/REUTERS

Mkutano wa leo wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa unafanyika baada ya mkutano wa Mwezi Machi uliokuwa na mabishano kati ya Blinken na mkuu wa masuala ya kigeni wa chama cha kikomunisti cha china Yang Jiechi juu ya sera , kuhusu tofauti kubwa za kisera kati ya mataifa hayo mawilii.

Blinken alisema serikali yake imeungana na washirika wake dhidi ya kile ilichokiita utawala wa mabavu wa China  na nguvu kubwa inayotumia ndani na nje ya nchi ikiwemo dhidi ya Taiwan, jamii ya walio wachache ya Uighur na Kusini mwa China.