Marekani,Kundus na wakimbizi magazetini
7 Oktoba 2013Tuanzie lakini Marekani ambako shughuli za serikali zimesita kwa siku ya sabaa mfululizo hii leo.Gazeti la "Stuttgarter Nachrichten" linaandika:
Vichwa mchungu wa siasa kali za mrengo wa kulia kutoka vuguvugu la Tea Party ndio wapinzani wakubwa wa mageuzi ya sekta ya afya.Walio wachache wanawakandamiza walio wengi.Hata kama mageuzi hayo ya karne yana walakini.Lakini ushupavu wao haumaanishi mwisho wa Marekani. Hayo hayawashughulishi hata kidogo..Wanachokilenga, ni kujipatia wingi wa kura katika mabaraza yote mawili, uchaguzi wa bunge la Marekani-Congress utakapoitishwa mwakani,pindi wakifanikiwa kuwashawishi wale wanaohamakishwa na "yanayotokea Washington".Lakini wataula na chua.Kwasababu raia wa Marekani wanawatwika wahafidhina jukumu la kufungwa taasisi za serikali.
Wanajeshi wa Ujerumani warejea nyumbani
Vikosi vya jeshi la shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Bundeswehr vimewakabidhi wenyewe waafghanistan jukumu la kusimamia usalama katika eneo la kaskazini la Kundus.Gazeti linalosomwa na wengi la "Bild" linatathmini mwongo mzima wa shughuli zao na kuandika:
Baada ya umwagaji damu wa mwongo mzima,vikosi vya jeshi la Ujerumani vinaondoka Kundus na kuliacha eneo hilo bila ya utulivu.Wataliban wanasonga mbele,serikali ya Afghanistan imeoza kwa rushwa na nchi hiyo inakurubia kutumbukia katika janga la vita vya wenyewe kwa wenyewe.Kwa machungu tumejionea shida iliyoko ya kueneza mfumo wetu wa demokrasia..Lakini Jeshi la shirikisho Bundeswehr limedhihirisha ujuzi na ustadi wake licha ya hali ngumu iliyoko.Vita nchini Afghanistan vimepelekea kuibuka kizazi kipya cha maafisa vijana,wenye ujuzi wa kupigana-maarifa ambayo wanajeshi wa Ujerumani hawatayasahau.Na Ujerumani imejifunza kuthamini kazi zinazofanywa na wanajeshi wake.Wanajeshi wa Ujerumani Bundeswehr wamesalimika na janga la risasi.
Wahariri wamezungumzia pia kuhusu huzuni zilizosababishwa na mwongo mzima wa shughuli za vikosi vya jeshi la shirikisho Bundeswehr huko Kundus. Gazeti la "Der neue Tag" linaandika:
Kile ambacho de Maizière ameshindwa kutambua ni kwamba:Ujerumani haiwezi hata kidogo kumeza machungu ya kupokea kila wakati majeneza ya watoto wao.Ndio maana kwa miaka sasa kilio ni kimoja tu,wanajeshi warejee haraka nyumbani ili kupunguza hasara ya maisha.Nchi inakabwa na kishindo cha wahanga na jamaa zao.Hata sifa za ushujaa hazisaidii kitu.Pengine de Maizière hataki kukiri:lakini ukweli ni kwamba Afghanistan ni mwisho na sio mwanzo wa kuwajibika wanajeshi wa Ujerumani katika viwanja vya mapigano ulimwenguni.
Ripoti yetu ya mwisho magazetini inahusu msiba wa wakimbizi baada ya mashua yao kuzama karibu na fukwe za Lampeduza nchini Italia.Gazeti la "Badische Neueste Nachrichten" linaandika:
Vipi kuwashughulikia wakimbizi,hilo linabidi kuwa suala linalostahiki kushughulikiwa na Umoja wa Ulaya.Sharti hapo ni kuwa na sera ya pamoja kuhusu haki ya ukimbizi-na hapo wanasiasa wanabidi wawajibike.Ufumbuzi unahitajika haraka kwasababu suala hili kwa muda mrefu sasa limekuwa likipuuzwa.Lakini kujijengea kuta na kutotolia maanani yanayotokea- mtindo huo hauwezekani tena hivi sasa.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman