Marekani,Taliban kufanya mazungumzo ana kwa ana mjini Doha
9 Oktoba 2021Ujumbe wa ngazi ya juu wa Marekani utakutana na wawakilishi wa Taliban matika mji mkuu wa Qatar Doha wikendi hii, kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Marekani iliyotolewa Ijumaa. Pande hizo mbili zimekuwa na mawasiliano tangu Taliban walipochukua madaraka nchini Afghanistan mwezi Agosti, lakini haya yatakuwa mazungumzo ya kwanza ya ana kwa ana.
Soma zaidi: Ujumbe wa Uingereza wakutana na maafisa wa Taliban
Marekani imepeleka ujumbe unaojumuisha maafisa wa wizara ya mambo ya nje, shirika la msaada wa kimataifa la Marekani, USAID pamoja na watu kutoka taasisi za kijasusi.
Yapi yatajadiliwa katika mkutano huo?
''Tutawashinikiza Taliban kuheshimu haki za raia wote wa Afghanistan, wakiwemo wanawake na wasichana, na kuunda serikali inayojumuisha makundi yote nchini humo,'' amesema msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani.
''Wakati Afghanistan ikikabiliwa na kitisho cha mporomoko wa uchumi na uwezekano wa janga la kibinadamu, tutawahimiza pia Taliban kuruhusu mashirika ya msaada wa kiutu kuyafikia maeneo yote bila vizuizi.'' Ameongeza msemaji huyo.
Soma zaidi: Mataifa makubwa yataka serikali ya wote Afghanistan
Njia salama kwa Wamarekani na washirika wao raia wa Afghanistan wanaotaka kuondoka nchini Afghanistan litakuwa suala jingine litakalojadiliwa.
Hali kadhalika,pande hizo mbili zitajadiliana kuhusu kitisha cha ugaidi na namna ya kuiepusha Afghanistan kugeuka tena ngome ya al-Qaida na makundi mengine ya kigaidi.
Marekani kuutambua utawala wa Taliban?
Wizara ya mambo ya nje mjini Washington imesisitiza kuwa mkutano huu haumaanishi kuwa Marekani inautambua utawala wa Taliban nchini Afghanistan.
''Mazungumzo haya hayamaanishi kuwatambua Taliban wala kuuhalalisha utawala wao,'' amesema msemaji wa wizara hiyo na kuongeza kuwa ''uhalali wowote utatokana na vitendo vya Taliban wenyewe.''
Mapema wiki hii maafisa wa Uingereza pia walifanya mazungumzo ya kwanza na Taliban mjini Kabul, mada ikijikita katika kuepusha mzozo wa kibinadamu, usalama na ugaidi, na haki za wanawake na watoto.
Hali ikoje Afghanistan wakati huu?
Tangu kuchukua udhibiti wa nchi katikati ya mwezi Agosti, wanamgambo hao wenye itikadi kali ya Kiislamu wamekuwa wakijaribu kuimarisha mamlaka yao katika maeneo yote ya nchi. Hata hivyo, wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa kutoka kwa kundi linalojiita Dola la Kiisalmu - IS, tawi linalojulikana ka IS ukanda wa Khorasan.
Ijumaa wiki hii, mripuko mkubwa katika msikiti kaskazini mwa Afghanistan ambao uliwalenga waumini wa madhehebu ya Shia, uliuwa na kujeruhi watu wasiopungua 100. Nchi hiyo pia inakabiliwa na hali mbaya kiuchumi, ikiarifiwa kuwa upungufu wa chakula umekithiri mnamo wiki chache zilizopita.
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa watu nusu milioni wamelazimika kuyahama makaazi yao nchini humo mnamo miezi ya hivi karibuni, na umeonya kuwa idadi hiyo itaongezeka haraka ikiwa uchumi na huduma za kijamii vitazidi kuzorota.
sri/rt (AFP, Reuters)