Maridhiano katika mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano
31 Januari 2018
Takriban magazeti yote ya Ujerumani yamejitokeza na kichwa cha maneno" "maridhiano katika mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano wa vyama vikuu-GroKo. Maoni lakini yanatofautiana kuhusiana na maridhiano hayo. Kuna wanaoyasifu na wanaoyatia ila. Gazeti la Flensburger Tageblatt linaandika:
Martin Schulz anahitaji ushindi. Na kwa namna hiyo Martin Schulz anatangaza ushindi ambao SPD hawajaupata hata kidogo. Kama jana katika suala la familia kujiunga pamoja na wakimbizi ambao hawana kinga kamili ya ukimbizi, ambapo vyama ndugu vya CDU/CSU na SPD wamekubaliana. Habari nzuri hapo ni kwamba kizingiti kikubwa katika mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano, kimeondolewa. Na habari mbaya kwa Martin Schulz ni kwamba: Maridhiano hayo yana rangi nyeusi, ikimaanisha kitambulisho cha rangi ya vyama ndugu vya CDU/CSU. Ikiwa mwenyekiti wa chama cha SPD atayapaka maridhiano hayo rangi nyekundu na kuyatangaza kuwa ushindi wa chama chake, hali hiyo itamaanisha chama chake kimeteremka kutoka hadhi ya mshirika mdogo na kusalia mshirika mchanga. Na hiyo haiwezi kuwa hadhi wanayojiwekea wana SPD. Martin Schulz anawapatia cha kusema wapinzani wake."
Mvutano haaujamalizika katika mazungumzo ya kuundwa serikali ya muungano GroKo
Gazeti la Stuttgarter Nachrichten linahisi mvutano haukumalizika. Gazeti linaendelea kuandika: "Hali ya kuvunjika moyo wafuasi wa pande zote mbili haiepukiki na inatishia kuzidi kuwapunguzia hamu ya kuunga mkono serikali ya muungano wa vyama vikuu-GroKo. CDU/CSU hawakutekeleza ahadi zao kwamba mpango wa kuruhusu kuungana familia za wakimbizi ambao hawajivunii kinga kamili ya ukimbizi usitishwe moja kwa moja, kwakuwa kuanzia mwezi wa Agosti familia 1000 za wakimbizi wataruhusiwa kuingia Ujerumani kwa mwezi, kama SPD walivyolazimisha. Wafuasi wa chama hicho lakini wanabidi waikumbuke sheria kama hiyo ambayo mwaka 2017 iliruhusu familia 66 tu kujiunga na familia zao. CDU/CSU na SPD wamekubaliana na mvutano unaendelea."
Kashfa ya kima kutumiwa katika majaribio ya maabara
Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu kashfa inayolikumba kampuni mashuhuri la magari nchini Ujerumani la Volks Wagen. Kampuni hilo linatuhumiwa kuwatumia kima kufanya majaribio ili kutambua kama kweli moshi unaotoka ndani ya magari una athari kwa afya za viumbe. Fadhaa na laana zimehanikiza humu nchini tangu kadhia hiyo ilipofichuliwa. Gazeti la "Landeszeitung" linaandika: "Mwenye makosa lazma apatikane. Tena haraka. Mkuu wa shughuli za kibiashara wa kampuni hilo Steg, ameshajiuzulu na pengine hakufanya vibaya. Ila kwa kujiuzulu yeye peke yake bado hewa haijatakata ipasavyo mjini Wolfsburg.Yadhihirika kana kwamba amejitolea mhanga tu. Na taarifa kwamba kampuni hilo limedhamiria kujua kima waliofanyiwa majaribio hali zao zikoje, ingawa zinawafanya watu wapumuwe kidogo lakini haitoshi.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri:Yusuf Saumu