1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Martin Fayulu asema wanajeshi wa EAC sio suluhisho kwa Kongo

Saleh Mwanamilongo
9 Novemba 2022

Mwanasiasa wa upinzani nchini Kongo Martin Fayulu, ameomba kusitishwa kwa mahusiano ya kidiploamisia baina ya Kongo na Rwanda pamoja na Uganda.

Martin Fayului kiongozi wa upinzani nchini Kongo
Martin Fayului kiongozi wa upinzani nchini KongoPicha: DW/S. Mwanamilongo

Martin Fayulu ambaye ameitembelea DW kufuatia ziara yake katika nchi kadhaa za Ulaya na Marekani amesema machafuko yanayoendelea mashariki mwa Kongo yanatokana na uongozi dhaifu wa Rais Tshisekedi, huku akilazimisha kusitishwa kwa uhusiano wa kidiploamisia baina ya Kongo na Rwanda pamoja na Uganda.

''Raia wa Kongo hawataki vita hivyo, raia wa Kongo hawataki uvamizi huo, raia hawataki umwagikaji damu huo. Na Tshisekedi hana chaguo jingine bali kutekeleza matwaka ya raia. Kitu ambacho Kongo inatakiwa kufanya ni kusitisha uhusiano wowote na nchi hizo na kuwasilisha malalamiko ya kuvamiwa kwake kwenye Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa.'' alisema Fayulu.

Fayulu anapinga kuletwa kwa wanajeshi wa nchi za Afrika Mashariki huko Kivu na Ituri. Anasema hilo sio suluhisho zuri. Wakati huo huo, anapendekeza kubadilishwa kwa muhula wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa, MONUSCO, ili kipewe nguvu zaidi ya kupigana.

''Uchaguzi ni wajibu wa kikatiba''

 

Wafuasi wa Martin Fayulu wapanga kuandamana wiki ijayo kupinga vitaPicha: John Wessels/AFP/Getty Images

Akigusia siasa za ndani ya nchi yake, Martin Fayulu ambaye anaendelea kudai kuwa ni raisi mteule wa Kongo, kutokana na kushinda kwenye uchaguzi wa 2018 kwa kupata asilimia 62, amesema tume ya uchaguzi lazima iitishe uchaguzi kama ilivyopangwa kikatiba na kwamba masharti kadhaa lazima yatekelezwe ili kuweko na uchaguzi bora na ambao matokeo yake yatakubalika na pande zote.

''Uchaguzi ni wajibu wa kikatiba. Baada ya kila miaka mitano ni lazima kuweko na uchaguzi. Tshisekedi hawezi kusalia madarakani baada ya muhula wake bila kuandaa uchaguzi. Lakini kabla ya kuitisha uchaguzi huo na kutangazwa kwa tarehe ya uchaguzi ni lazima pande zote husika zikubaliane kuhusu tume ya uchaguzi na mahakama ya katiba ambayo inatangaza mshindi wa uchaguzi wa rais, hivi sasa wote ni watu wa Tshisekedi.'' alisema Fayulu.

Mazungumzo ya pande husika

Alipoulizwa masharti ambayo uchaguzi utakuwa wa wazi, Martin Fayulu ameomba kuweko na mazungumzo baina ya viongozi vyama vikuu vya siasa. Hapo ametaja chama cha rais mstaafu Joseph Kabila, chama chake na kile cha kile Rais Tshisekedi na vile vile mashirika ya kiraia.

Martin Fayulu ametangaza kusitisha ziara yake hapa Ulaya ili kuandamana na raia wa Kinshasa ambao wanaomba kumalizika kwa vita huko mashariki mwa Kongo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW