Martine Aubry ashindwa: Francois Hollande ndiye mgombea wa urais
17 Oktoba 2011Bwana Francois Hollande aliibuka mshindi kwenye uchaguzi wa hapo jana Jumapili baada ya kuchuana na meya wa mji wa Lille na Waziri wa kazi wa zamani wa Ufaransa, Martine Aubry.
Hii ni mara ya kwanza kwa uchaguzi wa aina hiyo kufanyika nchini Ufaransa. Duru zinaeleza kuwa Francois Hollande aliye na msimamo wa wastani analiunga mkono suala la Ufaransa kuwa na ushirikiano wa karibu zaidi na mataifa mengine ya bara la Ulaya.
Pindi baada ya kuipiga kura yake, Bwana Hollande alisema kuwa chama chake cha Kisoshalisti kimeuanza mchakato wa kuhakikisha kuwa mgombea wake anaibuka mshindi katika uchaguzi wa rais ujao.
Itakumbukwa kuwa chama hicho kilipata ushindi wa aina hiyo kwa mara ya mwisho mwaka 1988. Kulingana na kura ya maoni, Francois Hollande huenda akampiku Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy endapo uchaguzi ungefanyika wakati huu.
Mwandishi: Mwadzaya, Thelma-ZPR