Marufuku kwa yeyote kutoka nje bila barakoa, Kenya
15 Aprili 2020Kwenye taarifa yake Inspekta mkuu wa polisi Hillary Mutyambai aliweka bayana kuwa wakenya wameshapewa muda wa kutosha kujipatia vazi hilo la kujikinga. Atakayepatikana bila barakoa mtaani atatozwa faini ya shilingi alfu 20 au kufungwa kwa muda usiozidi miezi sita au vyote.Itakumbukwa kuwa mwishoni mwa wiki iliyopita Waziri wa afya Mutahi Kagwe aliwasilisha kwenye gazeti rasmi la serikali adhabu ambazo zinaweza kutolewa kwa watakaokiuka sharia hiyo.
Wafanyakazi wa biashara zinazowavutia watu wengi kama vile maduka ya jumla, sehemu za kunyoa na kusuka nywele sharti wavae barakoa wanapowahudumia wateja.
Hata hivyo suala la ubora wa barakoa hizo linazua utata.Baadhi ya barakoa zinashonwa mitaani pasina kujali kanuni za usafi wala afya.
Kwa upande wake waziri wa biashara na viwanda Betty Maina alibainisha wiki iliyopita kuwa kampuni za kutengeza nguo za Kenya zina mali ghafi ya kutosha kushona barakoa miloni 6. Viwanda vya Kicotex kilichoko Kitui na Rivatex ya Eldoret ndivyo vilivyopewa wajibu wa kushona barakoa zitakazotimiza vigezo vya afya na kuwa bei nafuu..Wakenya wamekuwa wakiitolea wito serikali kuwapa barakoa bila malipo.
Kulingana na shirika la afya ulimwenguni barakoa zinaupunguza uwezekano wa kusambaza mate na majimaji kadhalika virusi vya corona kila mtu anapokohoa au kuzungumza.
Mwandishi: Thelma Mwadzaya, Nairobi