Wakosoaji wasema sheria inakiuka haki za binaadamu
11 Aprili 2016Wakati Rachid Nekkaz anapofika kwa karani wa kortini kulipa faini katika mji wa Evry, kusini mwa Ufaransa, ni kama anamtembelea rafiki yake wa muda mrefu, wanapiga gumzo na hata kutaniana.
Yeye ni mgeni wa mara kwa mara na sio mara yake ya kwanza kumlipia faini ya euro 150 mwanamke aliyetozwa faini hiyo kwa kufunika uso wake hadharani kutumia kitambaa cheusi au niqab inayotumiwa na waumini wa kike wa Kiislamu. Hii ni mara ya 1,089 kwa Nekkaz kulipa faini hiyo.
Nekkaz alianza kulipa faini hizo miaka mitano iliyopita, wakati marufuku hiyo ilipoanza kutekelezwa tarehe 11 mwezi Aprili, mwaka wa 2011.
Kuanzia wakati huo ametumia takriban euro 235,000 kuwalipia faini hiyo wanawake nchini Ufaransa na Ubelgiji ambako sheria kama hiyo ilianza kutekelezwa miezi kadhaa baada ya Ufaransa. Nchini Ubelgiji Nikkaz amelipa faini hizo mara 259.
Chini ya utawala wa rais Nicolas Sarkozy, Ufaransa ilikuwa taifa la kwanza la Ulaya kupitisha sheria iliyopiga marufuku wanawake wa Kiislamu kufunika nyuso zao hadharani, marufuku hiyo inajumuisha vitambaa vya kichwa, uvaaji wa barakoa, na hata kofia za kuendesha pikipiki au helmeti lakini kwa kiwango kikubwa sheria hii inawagusa wanawake wa Kiislamu wanaovaa niqab.
Sheria hiyo inajulikana kama marufuku ya Burqa ikimaanisha uvaliaji wa vazi la kufunika mwili mzima ambalo ni maarufu nchini Afghanistan na Kusini mwa Asia na Ufaransa lakini kwa uchache.
Sheria yaigawa jamii nchini Ufaransa.
Wale waliokubaliana na marufuku hiyo walisema kwamba inapingana na kanuni za Ufaransa za kuishi pamoja. Lakini baada ya miaka mitano je sheria hii imeweza kuwaleta watu pamoja kama walivyotarajiwa wabunge?
Mwanasosholojia na mtengeneza filamu Agnes De Feo, amesema hapana sheria hiyo imeitenganisha jamii badala ya kuiweka pamoja.
"Wanawake hawa wanatukanwa sana barabarani," alisema De Feo. Mwaka wa 2013 mwanamke aliyekuwa mjamzito alitoka mimba hiyo baada ya wanaume wawili kumvamia na kujaribu kukitoa kitambaa chake kichwani.
Baadhi ya wakosoaji wameiita sheria hiyo kama isiyofaa na inayokiuka haki za binaadamu. Aidha wabunge waliyoiunga mkono sheria hiyo wanasema itahakikisha utulivu miongoni mwa jamii na kuimarisha usalama wa kitaifa lakini hilo bado halijaonekana.
Olivier Roy, mtaalamu wa masuala ya Uislamu anasema Burqa haikuwa maarufu nchini Ufaransa, kwahiyo idadi ya Waislamu waishio huko hawakuipinga sheria kwa uwazi kwa sababu hawaulizi uwepo wa uhuru wa uvaaji wa burqa.
Roy anasema kumekuwa na hisia miongoni mwa Waislamu, waumini na wasio waumini kwamba marufuku hiyo ya burqa ni msukumo tu na shambulizi au maonevu dhidi ya Uislamu.
Mwandishi: Amina Abubakar
Mhariri:Iddi Ssessanga