1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marufuku ya safari dhidi ya Uingereza yaanza kuondolewa

Sylvia Mwehozi
23 Desemba 2020

Mataifa kadha ya Ulaya yameanza kulegeza marufuku ya safari iliyowekwa dhidi ya Uingereza katika juhudi za kukabiliana na kuenea kwa kirusi kipya cha corona wakati maafisa wa WHO wakitazamiwa kulijadili suala hilo.

UK LKW Stau auf der M20 vor dem Eurotunnel Terminal
Picha: Gareth Fuller/PA Wire/picture alliance

Kirusi kipya cha corona kimeikumba Uingereza na kuibua wasiwasi duniani kote wakati chanjo ya COVID-19 ikianza kutolewa. Hata hivyo, Halmashari kuu ya Ulaya siku ya Jumanne iliyataka mataifa ya Ulaya kuondoa marufuku ya safari iliyowekwa dhidi ya Uingereza katika siku za hivi karibuni. Aina mpya ya virusi, ambavyo pia vimegunduliwa kwa idadi ndogo mahali pengine, vinaonekana kusambaa kwa wepesi kuliko aina nyingine lakini wataalamu wanasema hakuna ushahidi kwamba ni hatari zaidi au vyenye ukinzani na chanjo.

Kugunduliwa kwa aina hiyo ya virusi kulizusha wasiwasi ambao ulisababisha nchi nyingi kusitisha safari za ndege na Uingereza na kutishia rapsha za safari wakati wa msimu wa sikukuu. Umoja wa Ulaya badala yake umetaka abiria wafanyiwe vipimo saa 72 kabla ya safari.

Ufaransa imeanza kuifungua mipaka yake na Uingereza hii leo, ingawa vipimo kwa ajili ya covid-19 vitahitajika. Uholanzi nayo imetangaza kuondoa marufuku hiyo lakini sio kwa abiria wote. Shirika la afya ulimwenguni WHO upande wa Ulaya, limesema wataalamu wake wanakutana leo Jumatano kujadili namna ya kushughulikia mlipuko huo, likisema kuzuia safari kwa ajili ya kudhibiti kuenea ni busara zaidi hadi pale kutakapopatikana habari njema.

Utoaji chanjo huko Israel Picha: Ronen Zvulun/REUTERS

Nchini Marekani Rais Donald Trump hapo jana aliukataa mpango mkubwa wa misaada ya kiuchumi ya covid uliopitishwa na bunge, akiutaja kuwa ni 'fedheha', ikiwa ni chini ya mwezi mmoja kabla aondoke madarakani na wakati mamilioni ya wamarekani wakiendelea kukabiliwa na janga la covid. Trump alidondosha bomu hilo katika taarifa iliyorekodiwa awali na kuwekwa katika ukurasa wa Twitter. Uamuzi wa Trump unakuja siku chache baada ya Warepublican na Wademocarts hatimaye kukubaliana juu ya mpango wa uokozi wa dola bilioni 900 unaokusudia kuzisaidia biashara na watu walioathirika na janga hilo.

 ''Ninalitaka bunge kuondoa mara moja vitu visivyo vya lazima katika muswada huu na wanitumie muswada unaofaa, la sivyo utawala unaofuata utalazimika kuja na mpango wa uokozi wa Covid. Na huenda utawala huo utakuwa wa kwangu na tutakamilisha,'' alisema Trump. 

Mataifa kadhaa yasitisha usafiri kutoka Uingereza kwa sababu ya aina mpya ya virusi vya corona

00:59

This browser does not support the video element.

Hapa Ujerumani maambukizi ya kila siku ya virusi vya corona yamefikia 962 siku ya Jumatano, ikiwa ni wiki moja baada ya taifa hilo kuzifunga shughuli nyingi za umma. Kulingana na takwimu za taasisi ya Robert Koch, idadi jumla ya vifo kwa hivi sasa imefikia 27,968

Nalo Baraza la juu la Kiislamu katika Umoja wa Falme za Kiarabu la Fatwa, limetoa uamuzi kwamba chanjo ya virusi vya corona itaruhusiwa kutolewa kwa Waislamu hata kama zitakuwa na nyama ya nguruwe. Uamuzi huo unafuatia ongezeko la wasiwasi kwamba matumizi ya nyama ya nguruwe ambayo ni kiungo cha kawaida katika utengenezaji wa chanjo kunaweza kudhoofisha utoaji wa chanjo miongoni mwa waislamu wanaochukulia bidhaa za nyama hiyo kuwa haramu.

Vyanzo: AFP/Reuters/AP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW