Mary Robinson Ziarani DRC
30 Aprili 2013Mary Robinson aliyekuwa rais wa Jamhuri ya Ireland kabla ya kupata wadhiwa wake mpya mwezi uliopita, amekuwa na changamoto kubwa ya kuhakikisha kuwa amani inapatikana katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambayo imekuwa ikikumbwa na mizozo kwa zaidi ya miongo miwili sasa.
"Wakaazi wa kanda hii ndio watakaofaidika na utekelezwaji wa makubaliano hayo ya matumaini. Nitaomba msaada wa jumla kwa mashirika ya kiraia, mashirika ya wanawake, vijana na makundi ya kidini ya kanda hii ili waweze kushawishi serikali zao katika utekelezwaji wa mkataba wa Addis Abeba,” Alisema Mary Robinson.
Mnamo February mwaka huu, mataifa 11 ya Afrika yalitia saini mkataba wa amani ambao ulinuia kumaliza vita na kuleta udhabiti katika Jamhuri ya kidemokrasia ya kongo, nchi ambayo imekuwa mara kwa mara ikishambuliwa na waasi mbali mbali ambao waliosababisha mauaji ya watu wengi na kuwabaka wanawake katika eneo hilo.
Mjumbe mpya maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kanda la maziwa makuu Mary Robinson ambaye alianzia ziara yake ya wiki moja barani Afrika mjini Kinshasa hapo jana anatazamiwa pia kuzuru Rwanda, Uganda, Burundi, na Afrika Kusini
Robinson atamalizia ziara hiyo katika makao makuu ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa Ethiopia.
M23 waanza mafunzo ya kijeshi
Huku hayo yakiarifiwa waasi wa M23 mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya kongo wamesema mamia ya wanajeshi wake wako katika mafunzo maalum ya kijeshi ili kukabiliana na kikosi kipya cha kulinda amani cha Umpoja wa Mataifa.
Akizungumza na shirika la habari la AFP msemaji wa jeshi la waasi hao Vianney Kazarama amesema takriban makamanda 462 wanapokea mafunzo hayo katika eneo la Rumangabo ambayo ni kambi kubwa ya jeshi katika mkoa wa Kivu ya Kaskazini. Kazarama amesema nia yao ni kuwaweka tayari kukabiliana na wanajeshi wa Umoja wa mataifa na kujilinda.
Kikosi cha Kulinda amani cha Umoja wa Mtaifa kitajumuisha wanajeshi 3000 kutoka mataifa ya kusini mwa Afrika na kuongozwa na Jenerali wa Tanzania.
Hata hivyo waasi wa M23 ambao serikali ya Kongo na tume ya wataalam ya Umoja wa Mataifa wamesema wanapata usaidizi kutoka kwa serikali ya Rwanda inatuhumiwa kwa kuhusika na visa kadhaa vya uhalifu katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo hatua iliowafanya vipongozi wake kuekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa.
Mwandishi: Amina Abubakar
Mhariri: Daniel Gakuba