1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maseneta Marekani kujadili sera za usalama mipakani

Isaac Gamba
10 Januari 2017

Maseneta  nchini Marekani wanatarajia kumshinikiza Jenerali John Kelly ambaye ni chaguo la Rais Mteule wa Marekani Donald Trump katika kuongoza wizara ya mambo ya ndani ya nchi hiyo juu ya mipango inayohusina na usalama.

USA Donald Trump in Manchester
Picha: Reuters/C. Allegri

Kuthibitishwa kwa Jenerali Kelly hakuna mashaka yoyote, lakini wajumbe wa kamati ya usalama wa ndani pamoja na masuala mengine ya serikali wanatarajia kutumia siku ya leo kujadili juu ya sera nzito zinazohusiana na masuala ya uhamiaji pamoja na usalama mipakani ambazo zilichukua uzito mkubwa wakati wa kampeni za urais nchini humo.

Jenerali Kelly ni mmoja kati ya majenerali wastaafu walioteuliwa na Donald Trump kuongoza nafasi za juu katika serikali ijayo ya kiongozi huyo na anaonekana kukubalika katika vyama vyote viwili vikubwa nchini humo vya Democrats na Republican kutokana na uzoefu wake kijeshi ambao utasaidia kufanikisha majukumu yake katika wizara hiyo ya mambo ya ndani.

Amewahi pia kuongoza kikosi cha jeshi nchini humo kilichoko katika jimbo la Florida ambacho kinashirikiana na wizara ya usalama wa ndani nchini humo katika kudhibiti usafirishaji haramu wa binadamu pamoja na madawa ya kulevya.

 Kikosi hicho cha jeshi pia kimekuwa kikifanya kazi kwa kushirikiana na idara ya uhamiaji ambayo ni sehemu ya wizara ya usalama wa ndani kuwasaidia watoto ambao hawana wasindikizaji wanaojaribu kuvuka mpaka kutoka Amerika ya Kati kuingia nchini Marekani.

Jenerali Kelly alijiunga na jeshi la nchi hiyo mnamo mwaka 1970 na ni miongoni mwa wanajeshi wa zamani wa nchi hiyo waliowahi kushiriki katika operesheni ya kivita nchini Iraq huku pia akiwa ni afisa wa ngazi ya juu kijeshi nchini humo kuwahi kupoteza kijana wake wa kiume ambaye pia alikuwa mwanajeshi wakati wa operesheni ya kijeshi nchini Iraq au Afghanistan.

Jenerali Kelly atakuwa ni mtu wa tano kuongoza idara hiyo ambayo inahusisha pia taasisi ambazo zinahusika na masuala ya kiusalama ikiwa ni pamoja na kumlinda rais, kuchukua hatua wakati majanga yanapotokea, kusimamia utekelezaji wa sheria za uhamiaji, kulinda mipaka pamoja na kuzuia usafirishaji wa madawa ya kulevya.

Republican yakosoa utawala wa Obama katika kushughulikia usalama mipakani

Jenerali mstaafu Marekani John KellyPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Balce Ceneta

Warepublican kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamika kuwa Rais Barack Obama ameshindwa kuchukua hatua katika kusimamia utekelezaji wa sheria za uhamiaji na wamekuwa wakiunga mkono mapendekezo ya Donald Trump yanayolenga kukabiliana na mapungufu hayo wanayodai hayakushughukiwa ipasavyo na utawala wa Rais Obama.

Rais Mteule Donald Trump ameapa kuwafukuza mamilioni ya wahamiaji wanaoishi nchini Marekani kinyume cha sheria  hususani wanaojihusisha na uhalifu, hivyo Jenerali Kelly huenda akabanwa kutoa maoni yake ni kwa jinsi gani atatekeleza kwa vitendo ahadi hiyo ya Donald Trump.

Wakati huo huo, jamii ya wanasheria nchini Marekani imekuwa ikijadili juu ya hatua ya Trump kumteua mkwe wake wa kiume Jared Kushner kuwa mshauri wake mwandamizi katika ikulu ya White House iwapo itakuwa imekwenda kinyume na sheria za nchi hiyo. Hata hivyo kamati ya mpito ya Trump imetetea hatua hiyo na kusema hakuna kipingamizi chochote kisheria kinachotokana na uteuzi huo.

Mwandishi:Isaac Gamba/ AP

Mhariri: Grace Patricia Kabogo