1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maseneta Urusi waidhinisha mswada kuwabinya wakosoaji

2 Juni 2021

Baraza la seneti Urusi limepitisha kwa wingi mswada wa sheria unaotarajiwa kutumiwa kuwapiga marufuku washirika wa mkosoaji wa serikali Alexei Navalny kushiriki katika uchaguzi, hatua ya karibuni ya ukandamiza upinzani

Russland Föderationsrat
Picha: Mikhail Tereshchenko/TASS/dpa/picture alliance

Mswada huo, uliopitishwa kwa kiasi kikubwa na Baraza la Shirikisho, huenda ukawazuia viongozi, wafadhili na wanachama wa kawaida wa makundi yanayozingatiwa kuwa ya itikadi kali, kugombea katika uchaguzi wa Bunge. Jumla ya maseneta 146 waliunga mkono mswada huo, wakati mmoja akipinga na mmoja akijizuia kupiga kura. Mswada huo utahitaji kusainiwa na Putin kabla ya kuwa sheria.

Mahakama ya Urusi inafikiria iwapo itauorodhesha mtandao wa kisiasa wa Navalny kuwa shirika la kigaidi na huenda uamuzi ukafanywa wiki ijayo. Wakosoaji wa Rais Vladmir Putin wanasema maafisa wa Urusi wanatanua kampeni dhidi ya upinzani kabla ya uchaguzi wa Bunge unaopangwa Septemba mwaka huu.

Mbunge wa zamani wa upinzani Gudkov anazuiliwaPicha: Alexander Shcherbak/TASS/imago images

Baada ya Navalny kufungwa jela na wengi wa washirika wake kukamatwa, wanaharakati wawili zaidi, Dmitry Gudkov na Andrei Pivovarov, wakakamatwa katika siku mbili zilizopita.

Soma pia: Urusi yamkamata mkosoaji mwingine wa Kremlin

Pivovarov, mkurugenzi mkuu wa zamani wa Open Russia, kikundi kilichovunjwa cha kupigania demokrasia, aliondolewa kwenye ndege akiwa njiani kwenda Warsaw Jumatatu usiku. Pivovarov mwenye umri wa miaka 39 anakabiliwa na kifungo cha hadi miaka sita jela kwa kujihusisha na kundi lisilofaa. Mahakama imeamuru awekwe kizuizini kwa miezi miwili akisubiri kesi yake. Msemaji wa Putin, Dmitry Peskov, amesema Ikulu haihusiki na ukandamizaji unaofanywa na mamlaka dhidi ya upinzani. "Kwanza, shinikizo la maafisa wa Urusi dhidi ya viongozi wa upinzani halihusiki kwa vyovyote na kuanza kwa Jukwaa la Kiuchumi la Kimataifa la mjini St Petersburg. Pili, haliwezi kuhusishwa na baadhi ya malalamiko ya kisiasa, kwa sababu baadhi ya tuhuma tulizosoma na kuletwa na vyombo vya sheria, hayana uhusiano wowote na siasa. tatu, hilo halituhusu, bali ni swali linalowahusu maafisa wa utekelezwaji wa sheria."

Hapo jana, polisi ilimkamata Gudkov baada ya kufanya msako katika makazi ya washirika na jamaa zake. Mbunge huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 41 anakabiliwa na kifungo cha hadi miaka mitano jela kwa madai ya kushindwa kulipa deni chini ya makubaliano ya zamani ya ukodishaji.

AFP