1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashabiki wa Bayern kurejea uwanjani ila vizuizi bado vipo

26 Januari 2022

Bayern Munich itacheza mechi yao ijayo ya nyumbani katika Bundesliga dhidi ya RB Leipzig Februari 5 mbele ya mashabiki 10,000 baada ya jimbo la Bavaria kuruhusu asilimia 25 ya mashabiki viwanjani

Fußball Bundesliga | FC Bayern München vs. Borussia Mönchengladbach | Deutscher Meister
Picha: Alexander Hassenstein/Getty Images

Bayern Munich itacheza mechi yao ijayo ya nyumbani katika Bundesliga dhidi ya RB Leipzig Februari 5 mbele ya mashabiki 10,000 baada ya jimbo la kusini mwa Ujerumani la Bavaria kutangaza kuwa viwanja wa mpira vya eneo hilo vinaweza kuruhusu asilimia 25 ya mashabiki, na hadi idadi ya juu ya watazamaji 10,000.

Mechi katika jimbo la Bavaria, zikiwemo za timu za Bundesliga Greuther Fürth na Augsburg, za ligi daraja la pili Nuremberg na Ingolstadt, daraja la tatu 1860 Munich na Würzburger Kickers, zitachezwa chini ya mazingira ya sheria ya "2G+" (waliopewa chanjo au kupona, pamoja na kipimo cha kuonyesha hauna maambukizi au chanjo ya nyongeza), na ulazima wa kuvaa maski za FFP2 na marufuku ya kuuza pombe.

Watzke atafakari kuchukua hatua ya kisheria Picha: picture-alliance/Camera4

Bavaria na waziri mkuu wake Markus Söder wamefanya maamuzi yao wenyewe kuhusu hilo. Mechi za kandanda na michezo mingine ya kulipwa kwingineko Ujerumani itaendelea bila mashabiki viwanjani, baada ya Kansela Olaf na mawaziri wakuu wengine wa majimbo kuamua kutoubadilisha pakubwa mkakati wa saa wa nchi katika vita dhidi ya virusi vya corona.

Watzke wa Borussia Dortmund atafakari kwenda mahakamani

Lakini wakati Bayern Munich na jirani zake watawakaribisha maelfu ya mashabiki viwanjani, mechi katika jimbo la North Rhine-Westphalia itabaki kuwa na mashabiki 750 pekee – licha ya jimbo hilo kuwa na viwanja vikubwa kabisa Ujerumani, mjini Dortmund, Cologne, Gelsenkirchen, Mönchegladbach, Düsseldorf na maeneo mengine.

Afisa mkuu mtendaji wa Borussia Dortmund Hans-Joachim Watzke ameelezea wasiwasi wake mara kadhaa na hata anazingatia kuchukua hatua ya kisheria.

"Tunafuatilia kwa karibu hatua zilizopitishwa na jimbo la NRW na kuona kama tunaweza kuomba zichunguzwe." Aliliambia shirika la habari la dpa. "inauma sana kwamba wengi wa washiriki wa mkutano wa mawaziri wakuu wa majimbo bado tu wanafikiria kuhusu vizuizi baada ya miaka miwili na sio kuhusu uwezekano wa kufanya maamuzi yenye mantiki.”

Borussia Dortmund hupoteza karibu euro milioni 4 kwa kila mechi inayochezwa bila mashabiki katika uwanja wao wa Westfalenstadion wenye uwezo wa mashabiki 83,000.

Chanzo: mashirika