1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Romania na Ukraine zapigwa faini na UEFA

21 Septemba 2023

Shirikisho la Soka barani Ulaya (UEFA) limekiwekea vikwazo chama cha soka nchini Romania baada ya mashabiki wa taifa hilo kuimba nyimbo zinazoiunga mkono Serbia wakati wa mechi ya kufuzu kwa Euro 2024 dhidi ya Kosovo

Fußball Logo UEFA Euro 2024 in Deutschland
Mashindano ya mataifa barani Ulaya yatachezwa mwakani nchini Ujerumani.Picha: Michael Sohn/AP/picture alliance

Shirikisho la Soka barani Ulaya (UEFA) limekiwekea vikwazo chama cha soka nchini Romania baada ya mashabiki wa taifa hilo kuimba nyimbo zinazoiunga mkono Serbia wakati wa mechi ya kufuzu kwa Euro 2024 dhidi ya Kosovo wiki iliyopita, bodi inayosimamia soka ya Ulaya imesema.

Mechi ya Septemba 12 mjini Bucharest ilisitishwa kwa dakika 50 baada ya baadhi ya mashabiki wa wa timu ya taifa ya Romania kuimba, "Serbia Serbia" huku wakibeba mabango yanayosomeka  'Kosovo ni Serbia'.

Soma zaidi: Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu bila ya Messi na Ronaldo

Kosovo ilitangazia uhuru wake kutoka Serbia mwaka wa 2008 na ilipata kutambuliwa na zaidi ya nchi 100 ulimwenguni, lakini sio na Romania.

Chama cha soka cha Romania(FRF) kimetozwa faini ya euro 40,000 na UEFA na kuamuriwa kwamba  mchezo unaofuata wa nyumbani wa Romania wa kufuzu Euro dhidi ya Andorra mnamo tarehe 15 mjini Bucharest uchezwe bila mashabiki.

Timu ya taifa ya Ukraine haijacheza nchini mwao tangu mwaka 2022 baada ya uvamizi wa Urusi nchini humo.Picha: David Davies/empics/picture alliance

Kwa upande mwingine, Shirikisho la Soka la Ukraine (UAF) limetozwa faini ya euro 20,000 na UEFA kwa kile kilichoitwa  "tabia ya kibaguzi" ya mashabiki wake wakati wa mechi ya kufuzu kwa Michuano ya Euro kati ya Ukraine na Uingereza mnamo Septemba 9 mjini Wroclaw, Poland, ambapo mashabiki walionesha bendera zenye alama za mrengo wa kulia.

UEFA imeamuru pia kufungwa kwa sehemu ya uwanja wa Prague uliokuwa mwenyeji wa mchezo ujao wa Ukraine dhidi ya Macedonia Kaskazini mnamo Oktoba 14. UAF pia imepigwa marufuku kuuza tiketi kwa mashabiki kwa ajili ya mchezo wake ujao wa ugenini huko Malta mnamo Oktoba 17.

Ukraine haijacheza nyumbani tangu ilipovamiwa na Urusi mnamo Februari 2022.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW