1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashahidi: Trump alitaka kujiunga na vurugu za Capitol Hill

Babu Abdalla29 Juni 2022

Msaidizi wa zamani wa Ikulu amesema aliyekuwa rais Donald Trump alijaribu kuchukua usukani wa gari linalombeba rais mnamo Januari 6, mwaka 2021 baada ya kikosi chake cha ulinzi kukataa kumpeleka katika majengo ya bunge.

Cassidy Hutchinson
Msaidizi wa zamani wa Ikulu Cassidy HutchinsonPicha: J. Scott Applewhite/AP/picture alliance

Msaidizi wa zamani wa Ikulu ya White House amesema aliyekuwa rais Donald Trump alijaribu kuchukua kwa nguvu usukani wa gari linalombeba rais mnamo Januari 6, mwaka 2021 baada ya kikosi chake cha ulinzi kukataa kumpeleka katika majengo ya bunge, ambapo wafuasi wake walikuwa wamelivamia bunge la Marekani.

Katika ushuhuda ambao umeushangaza ulimwengu, msaidizi wa zamani wa Ikulu ya White House Cassidy Hutchinson amesema aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump alipuzilia mbali hofu ya usalama kwamba baadhi ya wafuasi wake waliokuwa wamekusanyika wakati Trump alipokuwa anatoa hotuba nje ya Ikulu, walikuwa wamebeba bunduki aina ya AR-15.

Soma pia: Mashahidi: Trump alimshinikiza Pence kubatilisha matokeo

Bwana Trump, licha ya hatari ya wazi iliyoko, aliwataka maafisa wa usalama kuacha kuwakagua wafuasi wake waliofika kusikiliza hotuba yake ili umati huo uonekane mkubwa. 

Bi. Cassidy Hutchinson ambaye alikuwa msaidizi wa mkuu wa wafanyikazi wa Ikulu alimnukuu Trump akisema kwa hasira, "Ondoeni vifaa hivyo vya ukaguzi, watu hawa hawako hapa kunidhuru."

Trump aliwataka maafisa wa usalama kutowakagua wafuasi wake

Wafuasi wa Marekani wakiandamana mjini WashingtonPicha: John Minchillo/AP/picture alliance

Hutchinson, ambaye anatoa ushahidi mbele ya bunge la Marekani linalochunguza uvamizi wa majengo ya bunge Januari 6, amesema kauli hizo za Trump ziliwasilishwa kwake na Tony Ornato, afisa mkuu wa kitengo cha kumlinda rais cha Secret Service ambaye alikuwa ni naibu mkuu wa wafanyikazi wa Ikulu.

Viongozi duniani walaumu uvamizi wa majengo ya bunge na seneti nchini Marekani

01:59

This browser does not support the video element.

Hutchinson amesema "Nilikuwa ndani, nilikuwa karibu na sehemu walimokuwa wanazungumza na nilimsikia rais akisema, sijali kama wamebeba silaha au la. Wawaache watu wangu, hawako hapa kunidhuru. Ondoeni hivyo vifaa vya ukaguzi. Wanaweza kuandamana kuelekea majengo ya bunge. Waacheni watu wangu, na muondoe huo upuzi."

Televisheni ya NBC na gazeti la New York Times, yaliyonukuu vyanzo kutoka kitengo cha kumlinda rais, yamesema mkuu wa kitengo cha ulinzi wa Trump, Robert Engel na dereva wa Trump walikuwa tayari kutoa ushahidi chini ya kiapo kwamba rais huyo wa zamani hakujaribu kuchukua usukani wa gari la rais.

Soma pia: Trump na washirika wake huenda walitenda uhalifu

Hutchinson ameeleza kuwa Engel alikuwepo wakati Ornato alipokuwa akielezea kilichotokea wakati huo.

New York Times na CNN, yakinukuu vyanzo ambavyo hawakuvitaja, yamesema Ornato afisa mkuu wa kitengo cha kumlinda rais cha Secret Service alikanusha kuwa Trump alijaribu kuliendesha mwenyewe gari la rais na kujiunga na wafuasi wake waliovamia majengo ya bunge, na kwamba yuko tayari kutoa ushahidi.

Hutchinson ameendelea kueleza mazungumzo kati yake na Ornato aliyesisitiza kuwa Bwana Trump aliwapa wakati mgumu walinzi wake, ambao walikuwa wanamuhimiza arudi Ikulu badala ya kujiunga na wafuasi wake kwenye maandamano.

Wafuasi wa Trump waliokuwa na hasira, walichochewa na madai ya kiongozi huyo yasiokuwa na msingi kwamba uchaguzi wa mwaka 2020 haukufanyika kwa njia ya haki , na kwamba kushindwa kwake kulitokana na udanganyifu.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW