1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashaka yaugubika mkutano wa kilele Brussels

17 Machi 2016

Viongozi wa Úmoja wa Ulaya waanza mkutano wao huku mashaka yakianza kujitokeza juu ya uwezekano wa kupatikana makubaliano na Uturuki.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya na Uturuki katika mkutano Brussels
Viongozi wa Umoja wa Ulaya na Uturuki katika mkutano BrusselsPicha: picture-alliance/dpa/O. Hoslet/Pool

Rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean Claude Junker amesema anaimani kwamba viongozi wa Jumuiya hiyo pamoja na Uturuki watafikia makubaliano katika mkutano wa kilele wa siku mbili wenye lengo la kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa wakimbizi wanaomiminika barani Ulaya miongoni mwa masuala mengine.

Kabla ya kukutana viongozi hao mchana wa leo mjini Brussels Junker alikuwa na mkutano na waandishi wa habari ambapo alizungumzia matarajio yake kwamba anahakika makubaliano yatafikiwa kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki leo au kesho. Juu ya hilo aliongeza kwamba anaamini makubaliano hayo yataheshimu sheria za Umoja wa Ulaya na mkataba wa Geneva. Kwa upande wake rais wa baraza la Ulaya Donald Tusk amesika akiwa na mashaka zaidi kuhusiana na kikao hicho akisema.

''Makubaliano ni lazima yakubalike kwa wanachama wote 28 wa Umoja wa Ulaya haijalishi ni mwanachama mdogo au mkubwa.Pili makubaliano hayo lazima yazingatie kikamilifu sheria za Ulaya na za kimataifa.Na tatu yanabidi yaweze kusaidia kwa dhati kutatua mgogoro wa wakimbizi na kuchangia katika mkakati wetu ambao ni pamoja na kuturudisha katika makubaliano ya schengen na kumaliza wimbi hili kupitia sera,kutoa msaada wa kibinadamu kwa Ugirikji kuziunga mkono nchi za Magharibi za Balkan na bila shaka kuimarisha ushirikiano na Uturuki''

Tamko la Tusk limeonekana wazi kulenga kuzipa nguvu na usemi nchi kama Cyprus ambayo inapinga kuharakishwa mazungumzo ya Uturuki kutaka kujiunga na Umoja huo hadi pale setrikali ya mjini Ankara itakapotimiza wajibu wake. Cyprus imeshasema itatumia kura ya Turufu kuzuia makubaliano hayo ya Umoja wa Ulaya na Uturuki. Mgogoro wa wakimbizi hata hivyo unazifanya nchi za Umoja wa Ulaya kuitegemea kwa hivi sasa kwa kiasi kikubwa Uturuki iingie katika makubaliano ya kuufunga mipaka yake ya eneo la pwani na kuzuia wimbi la wakimbizi wanaoendeleea kumiminika kuelekea Ulaya.

Wakimbizi wakiwa katika mpaka Kati ya Ugiriki na Macedonia,IdomeniPicha: Getty Images/AFP/D. Dilkoff

Tusk ametabiri kwamba mazungumzo ya leo na kesho yatakuwa magumu na hasa kwakuwa ni lazima makubaliano hayo tayari yanapingwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa na ya haki za binadamu.

Wakati huo huo, rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean- Claude Juncker amesema kuondoka kwa vikosi vya kijeshi vya Urusi nchini Syria ni jambo linalokaribishwa na litasaidia kupunguza mmiminiko wa wakimbizi, unaoisababishia Ulaya mgogoro mkubwa wa wahamiaji kuwahi kushuhudiwa kwa miongo mingi. Rais Vladimir Putin wa Urusi aliushangaza ulimwengu mapema wiki hii alipoamuru majeshi yake yarudi nyumbani, baada ya kampeni ya mashambulizi ya anga ya tokea Septemba kuusaidia Utawala wa Rais wa Syria Bashar al-Assad kupambana na makundi yenye silaha yanayoupinga utawala huo.

Ama kwa upande mwingine rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean Claude Junker amezungumzia juu ya hatua ya Ukraine kufanya mageuzi muhimu kwa ajili ya chombo hicho cha juu katika Umoja wa Ulaya kutoa uamuzi kwamba mwezi ujao raia wa Ukraine wataruhusiwa kupewa viza ya kusafiri kwa uhuru katika nchi zote wanachama wa Umoja huo. Kimsingi Umoja huo wa Ulaya umetumia nafasi hiyo kuondoa masharti ya kupata viza raia wa Ukraine kwa muda mfupi katika nchi za eneo la mipaka huru la Schengen kama kitendo cha kushawishi kufanyika mageuzi katika nchi majirani zake za Ulaya Mashariki.Hii leo akiwa Brussels rais Petro Poroshenko wa Ukraine alisema nchi yake imetimiza wajibu wake wa kufanya mageuzi katika maeneo kadhaa ya kukabiliana na rushwa na ufisadi,sheria pamoja na masuala ya ndani.

Mwandishi: Saumu Mwasimba, rtr

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW