Mashambulio dhidi ya Libya yasitishwe kwa muda
22 Juni 2011Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Franco Frattini ameiambia kamati ya bunge mjini Rome kuwa kuna haja ya kusitisha uhasama nchini Libya, ili misaada ya kiutu iweze kufikishwa kwa raia wa kawaida. Vile vile jitahada za kumaliza mgogoro huo na kuanzisha mazungumzo rasmi ya amani, ziendelee. Kwa maoni yake, ni halali kutaka maelezo zaidi kuhusu matokeo ya operesheni ya NATO. Yeye amelaani makosa yaliyosababisha vifo vya raia wa kawaida wa Libya. Amesema, ni dhahiri kuwa hilo sio lengo la operesheni ya NATO.
Lakini Katibu Mkuu wa NATO Anders Fogh Rasmussen , bila ya kuitaja Italia, amesema NATO itaendelea na kampeni yake ya kijeshi nchini Libya. Amesema, operesheni hiyo ikisitishwa, basi raia wengi zaidi huenda wakapoteza maisha yao. Hata Ufaransa inayoshika bendera katika operesheni za kijeshi dhidi ya Muammar Gaddafi, imepinga kabisa uwezekano wa kusitisha kwa muda kampeni ya Libya. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Ufaransa, Bernard Valero amesema, operesheni hiyo ikisitishwa kwa muda, Gaddafi ataitumia fursa hiyo kujipanga upya na raia wa kawaida ndio watakaoumia.
Hata hivyo, NATO imepaswa kutetea operesheni yake ya anga, baada ya kukiri kuwa bomu lake lilikosea shabaha yake. Kwa mujibu wa serikali ya Libya raia tisa waliuawa katika shambulio la NATO mjini Tripoli. Kosa hilo ni fedheha kwa operesheni inayojivunia kuwalinda raia wa Libya. Hata wiki iliyopita, ndege za NATO kwa makosa zilishambulia mlolongo wa magari ya waasi wa Libya.
Mkuu wa Umoja wa Nchi za Kiarabu, Amr Mussa anaeacha wadhifa huo ameeleza wasiwasi wake kuhusu kampeni ya NATO. Mwanadiplomasia huyo wa Kimsri, alikuwa na dhima muhimu kuzishawishi nchi za Kiarabu kuunga mkono azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lililoidhinisha mashambulio ya NATO. Lakini katika mahojiano yake na gazeti la Kingereza "Guardian" ametoa mwito wa kusitisha mashambulio. Amesema majadiliano yanapaswa kuanzishwa, kutafuta ufumbuzi wa kisiasa hata ikiwa Gaddafi yungali madarakani. Amr Mussa ameeleza kinagaubaga kuwa kampeni ya kijeshi huenda isifanikiwe.
Kwa upande mwingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa China Yang Jiechi, amesema China inalitambua Baraza la Mpito la Kitaifa la waasi wa Libya, kama mshirika muhimu wa majadiliano. Alitamka hayo leo hii, baada ya kukutana na kiongozi mwandamizi wa waasi wa Libya, Mahmud Jibril mjini Beijing. Mara kwa mara, China hupinga hatua inazodhani kuwa ni kuingilia mambo ya ndani ya nchi zingine. Lakini majuma ya hivi karibuni, imekutana na waasi wa Libya - hatua inayotazamwa kama ishara ya China kutaka kusaidia kuumaliza mgogoro katika nchi yenye utajiri wa mafuta barani Afrika, ambako ina maslahi makubwa ya kiuchumi.
Mwandishi: Martin,Prema/afpe
Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed