Mashambulio Syria: Raia 10 wauawa miongoni mwao watoto wanne
30 Julai 2021Kwa mujibu wa taarifa ya wakaazi wa jimbo la Deraa na jeshi la Syria, waasi walifanya mfululizo wa mashambulio kwenye sehemu hiyo kwa kutumia makombora. Mashambulio hayo kwenye vituo vya kijeshi yamevuruga shughuli za usafirishaji pia kwenye lango la kupitishia mizigo kati ya Syria na Lebanon.
Kwa mujibu wa taarifa ya waasi miji na vijiji muhimu karibu na mpaka wa Jordan vimetekwa. Majeshi ya serikali yamepeleka vikosi zaidi vya brigedi maalumu inayoongozwa na ndugu yake rais Bashar al-Assad.Taarifa hiyo inathibitisha habari zilizotolewa na wanajeshi waliolikimbia jeshi la serikali.
Waasi walifanya hujuma baada ya majeshi ya serikali kuendesha operesheni ya alfajiri kwenye kituo kinachoshikiliwa na waasi hao katika mji wa Deraa. Kwa mujibu wa taarifa ya shirika la habari la Ujerumani DPA raia 10 wameuawa miongoni mwao watoto wanne.
Majeshi ya serikali ya Syria yakisaidiwa na ndege za Urusi na wanamgambo wa Iran yalifanikiwa kulikomboa jimbo hilo muhimu la kusini linalopakana na Jordan na milima ya Golan mnamo mwaka 2018. Vyombo vya habari vya serikali vimeripoti kwamba magaidi wameishambulia hospitali kuu ya jiji la Deraa na kwamba mamia ya raia walihamishwa kutoka kwenye maeneo yanayoshikiliwa pamoja na waasi ambao hapo awali walikubali kusalimisha silaha zao nzito kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa kutokana na upatanishi wa Urusi.
Shirika la haki za binaadamu la Syria lenye makao yake nchini Uingereza limesema mapigano makali yalitokea hapo jana kwenye mji wa Deraa. Kwa mujibu wa shirika hilo askari wapatao 40 wa serikali pamoja na wanamgambo wanaoshirikiana nao walitekwa na waasi.
Majeshi ya serikali yameuzingira mji wa Deraa tangu wiki iliyopita ili kuwalazimisha waasi kuweka silaha chini. Mji wa Deraa ulikuwa kitovu cha maandaano ya kuupinga utawala wa Assad yaliyosambaa nchini Syria Kote.
Vyanzo://RTRE/DPA