1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulio ya Dortmund kushughulikiwa Karlsruhe

Oumilkheir Hamidou
12 Aprili 2017

Polisi wanachunguza kama shambulio dhidi ya basi ya timu ya Borussia Dortmund lilikuwa la kigaidi au la. Ofisi ya mwendesha mashitaka mkuu mjini Karlsruhe inashughulikia kadhia hiyo.

Dortmund -  nach Bombenanschlag auf BVB-Bus
Picha: picture-alliance/Nordphoto/Rauch

Miripuko mitatu iliyotokea jana usiku, muda mfupi kabla ya duru ya kwanza ya robo fainali kati ya Dortmund na Monaco inaathiri pia pambano jengine la kusisimua litakalofanyika leo usiku kati ya  Bayern Munich na Real Madrid.

Kwa mujibu wa gazeti la mjini Munich, Süddeutsche Zeitung, vituo vya matangazo vya WDR, na NDR pamoja pia na shirika la habari la Ujerumani dpa, barua iliyogunduliwa katika eneo  shambulio hilo lilikotokea na kuandikwa "Bismillahi Rahmani Rahim" ikimaanisha kwa kiswahili" Kwa jina la Mwenye enzi Mungu, mwenye rehema kubwa kubwa na mwenye rehema ndogo ndogo", inazungumzia kuhusu kujiunga Ujerumani  na ushirika dhidi ya kundi linalojiita dola la kiislamu IS pamoja pia na shambulio katika soko la Krismasi mjini Berlin ambalo kundi hilo la kigaidi linadai kuhusika.

Kwa mujibu wa gazeti la Süddeutsche polisi wanaonya dhidi ya watu kufamaya pupa, wanasema "kuna uwezekano kwamba wale waliofanya mashambulio hayo wanataka kuwakanganya watu kwa kutoa maelezo ya uwongo.

Ofisi za mwendesha mashitaka mkuu wa shirikisho mjini KarlsruhePicha: picture-alliance/dpa/U. Anspach

Njia zote zinachunguzwa

Ofisi ya mwendesha mashitaka mkuu wa shirikisho, ambayo ndio pekee yenye haki ya kushughulikia masuala ya ugaidi imesema leo asubuhi inashughulikia kisa hicho - ingawa haikutaja inafuata njia gani. Mkutano na waandishi habari utaitishwa saa nane za mchana kwa saa za Ulaya ya kati mjini Karlsruhe.

Kuanzia jana usiku polisi wameelekeza uchunguzi wao katika barua iliyogunduliwa mahala mashambulio hayo yalikotokea, lakini polisi hawakuzungumzia kilichoandikwa. Shirika la habari la dpa linazungumzia kwa upande wake kuhusu barua ya pili iliyochapishwa mtandaoni na kuwahusisha wafuasi wa vuguvugu linalopinga ufashisti.

Hatua za usalama zimeimarishwa hii leo katika mji wa Dortmund na maeneo ya karibu na uwanja wa michezo licha ya kwamba ulinzi tokea hapo ni mkali kufuatia mashambulio ya mwaka jana nchini Ujerumani na hasa lile dhidi ya soko la Krismasi mjini Berlin ambapo watu 12 waliuwawa na 48 kujeruhiwa.

Mwenyekiti wa timu ya Borussia Dortmund Reinhard RauballPicha: picture-alliance/dpa/R. Jensen

Dortmund yasifu mshikamano kati ya wanadimba

Dortmund inayokamata nafasi ya nne ya orodha ya matokeo jumla ya ligi kuu Bundesliga na Monaco, ambao ni mabingwa wa ligi kuu ya Ufaransa watateremka uwanjani leo usiku baada ya  mchuano wao kuakhirishwa jana usiku.

Mwenyekiti wa timu ya Borussia Dortmund Reihard Rauball anasifu mshikamano miongoni mwa wanasoka na mashabiki wao na kusema:"amefurahi sana alipowasikia mashabiki wa Monaco wakipaza sauti na kuita Dortmund Dortmund. Mshikamano kama huu unakutikana katika spoti tu na hili ndilo jambo pekee la kutia moyo tulilolishuhudia jana. Katika michezo kuna uwezekano wa kushikamana, kuheshimiana na kusaidiana."

Kwa upande mwengine hatua za usalama zimeimarishwa mjini Munich kunakofanyika leo usiku mchuano wa robo fainali kati ya Bayern Munich na Real Madrid.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/SID/dpa/Reuters

Mhariri:Josephat Charo