Mashambulizi dhidi ya Wakristo wa Mashariki ya Kati yawagusa wahariri wa Ujerumani
3 Januari 2011Suala lililochukuwa nafasi zaidi, hata hivyo, ni hili la hatima ya Wakristo katika nchi za Mashariki ya Kati, kufuatia mashambulizi ya kigaidi katika nyumba zao za ibada, kwanza Iraq na baadaye Misri, mwishoni mwa mwaka uliopita.
Gazeti la Rheinishe Post linaandika kwamba Chama cha Christian Social Union (CSU) kimekasirishwa sana na namna jamii ya Kikristo inavyotendewa kwenye nchi hizi. Na sasa kiongozi wa chama hicho bungeni, Stefan Müller, anasema kwamba, kuanzia sasa, ni lazima Ujerumani izingatie ikiwa misaada ya kimaendeleo inayotoa, haiendi kwa nchi inayokandamiza Wakristo. Na ikitokea kwamba nchi haiwapi haki yao Wakristo, basi msaada usielekezwe huko.
Lakini, wakati Stefan Müller akitaka chujio litumike kwenye utoaji wa misaada ya maendeleo, gazeti hilo hilo la Rheinische Post linamnukuu Waziri wa Uchumi wa Ujerumani, Dirk Niebel, kutoka chama cha kiliberali cha FDP, akisema kwamba, nchi yake itatumia miaka yake miwili kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhimiza misaada zaidi kwa Bara la Afrika.
"Lazima tulipe bara la Afrika nafasi kubwa zaidi ya kuendelea, kuliko ilivyokuwa hapo mwanzoni. Licha ya kuwa nchi 53 za bara hilo zinatafautiana sana na sisi, bado ziko karibu yetu, sio tu kijiografia, bali hata katika masuala ya usalama. Na kwa hivyo, ni wajibu wetu kuona kuwa zinaendelea." Amesema Waziri Niebel.
Mwisho ni maoni ya mhariri wa gazeti la Neue Osnabrücker kuhusu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, ambaye katika majira ya kiangazi ya mwaka huu wa 2011, huenda akagombea tena nafasi hiyo. Gazeti hilo linaandika gazeti kwamba tangu mwanzoni, Ban Ki Moon alikuwa ni mgombea ambaye hakupendelewa sana na Rais wa wakati huo wa Marekani, George W. Bush.
Lakini, kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita, Ban Ki Moon amejitahidi kufanya kazi na serikali ya Marekani, hata katika yale mambo ambayo, kimsingi, Umoja wa Mataifa unatafautiana na Marekani, kama suala la vita vyake nchini Afghanistan na Iraq.
Mtangulizi wake, Kofi Annan, alipata Tunzo ya Amani ya Nobel ya mwaka 2001, kwa msimamo wake wa kupigania amani. Bado haijajuilikana ikiwa naye Ban Ki Moon atapata nishani hiyo au la. bado.
Mwandishi: Mohammed Khelef
Mhariri: Othman Miraj